Pages

Thursday, November 7, 2013

‘Madudu’ yaibuliwa

mchome_342a8.jpg
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Profesa Sifuni Mchome
Wakati Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne nchi nzima ukiendelea, imebainika kuwa madaraja na alama mpya za ufaulu kwa shule za sekondari zilizotangazwa na Serikali hivi karibuni ni tofauti na zile zilizopendekezwa na Kamati Maalumu iliyoundwa kuchunguza suala hilo pamoja na zile zilizotolewa na makundi mbalimbali yaliyoshiriki kuandaa mfumo huo mpya.
Mbali na kwenda kinyume na maoni hayo, alama hizo zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kuwa na viwango vya chini vya ufaulu.
Alama hizo zilizotangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome zinaonyesha kwamba: A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19, huku alama endelevu za upimaji wa mwanafunzi shuleni (Continuous Assessment-CA) ikiwa ni 40 na mtihani wa mwisho ukichangia alama 60.
Kabla ya Serikali kutangaza alama hizo mpya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliunda Kamati Maalumu iliyopewa jukumu la kufanya uchunguzi na kuja na mapendekezo ya viwango vipya vya ufaulu na utaratibu wa CA.
Kamati hiyo ilifanya kazi hiyo na kukabidhi ripoti yake wizarani Septemba mwaka huu na mapendekezo yake kwenye upangaji wa alama hizo ilikuwa ni A= 80-100, B= 70-79, C= 50-59 D= 40- 49, E= 35- 39 na F= 0-34 huku wakitaka CA iwe alama 25.
Baada ya kuandaliwa kwa ripoti hiyo, Serikali ilitafuta maoni zaidi kutoka kwa wadau wengine kupitia makundi mbalimbali ambayo nayo yalitoa mapendekezo.
Kundi la kwanza lililotoa mapendekezo yake ni Jukwaa la Taasisi za Elimu za Serikali ambalo lilitaka ufaulu uanzie alama 40, kundi jingine ni Vyuo vya Watu Binafsi ambalo lilipendekeza ufaulu uanze alama 35 huku Wakuu wa Vyuo vya Serikali na Wakaguzi Wakuu wa Kanda wakitaka ufaulu uanzie alama 40 na CA iwe 30.
Ofisa mwandamizi kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini alisema kitaalamu CA hutakiwa kuwa chini ya alama ambayo inahesabika kuwa ndiyo ufaulu.
Alisema baada ya Serikali kupitisha mfumo ambao ufaulu unaanzia 20, ilitarajiwa CA kuwa chini ya 19 badala ya 40 iliyopitishwa na wizara.
Ufaulu wa chini
Kwa mujibu wa kitabu kinachoonyesha viwango vya ufaulu duniani kila mwaka cha International Qualification, baada ya Tanzania kutangaza alama hizo mpya, sasa inakuwa nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na alama za chini za ufaulu.
Nchi zinazofuatia kwa viwango vya chini baada ya Tanzania ni Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ambazo hata hivyo, viwango vyake vipo juu kwa kiwango kikubwa vikilinganishwa na vile vya Tanzania.
Kenya, Rwanda na Uganda kwa mfano, zinatumia mfumo unaojulikana kwa jina la Flexible Grade Range (mfumo wa kubadilika badilika) ambao viwango vya alama zake vipo kwenye asilimia tofauti na Tanzania ambayo inatumia mfumo usiobadilika wa Fixed Grade Range.
Kenya kwa mfano, viwango vyake ni A=70-100, B=60-69, C=50-59, D=40, 49 F=0-39. Viwango vya Rwanda ni A=90-100, B=80-89, C+=70-79, C=50-69, na F=0-49 na vya Uganda ni A=80-100, B+=70-79, B=60-69, C=50-59, D=45-49 na F=0-44.
Kwa mujibu wa kitabu hicho, DRC na Burundi ambazo zinatumia mfumo usiobadilika kama Tanzania, bado viwango vyake vya ufaulu vipo juu. Viwango vya nchi hizo vinafanana navyo ni: A=90-100, B+=80-89, B=70-79, C+=60-69, C50-59 na F=0-49.
Kwa Afrika, Misri na Ethiopia ndizo zenye viwango vikubwa zaidi vya ufaulu. Misri viwango vyake ni: A=90-100, B=80-89, C=65-79, D=50-64 na F=0-49 wakati Ethiopia ni A=90-100, B=80-89, C=60-79, D=50-59 na F=0-49. Miongoni mwa nchi zenye viwango vikubwa vya ufaulu duniani ni China ambavyo alama zake ni A=100-80, B=79-70, C=69-60, D=0-59. Mwanafunzi anayepata alama chini ya 60 huhesabika kuwa amefeli.
Kwa mfumo mpya hakuna kufeli
Katika kujaribu matumizi ya alama hizo mpya za ufaulu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliiagiza Necta kupanga matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012 na yale ya Kidato cha Sita mwaka 2013 kwa kutumia alama hizo.
Baada ya matokeo hayo kupangwa, ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne ulionekana kupanda na kufikia asilimia 93.74 kutoka asilimia 43 ambayo ndiyo idadi ya wanafunzi waliofaulu mwaka jana baada ya matokeo ya awali ambayo ufaulu wake ulikuwa asilimia 35 kufutwa na kupangwa upya.
Wanafunzi ambao wangefeli, ambao kwa mfumo wa sasa wanaitwa 'waliopata ufaulu usioridhisha' ni 23,285 sawa na asilimia 6.26 kutoka wanafunzi 210,846 sawa na asilimia 57 waliopata sifuri kwenye matokeo ya awali.
Kwa upande wa mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2013, mfumo huo mpya uliotolewa unaonyesha kuwa wanafunzi ambao wangefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu ni asilimia 99.67 kutoka asilimia 80 za matokeo ya awali na Daraja la Nne wangekuwa asilimia 0.27 kutoka asilimia 10.18 na wale wa sifuri wangekuwa ni wanafunzi 26 tu sawa na asilimia 0.06 kutoka wanafunzi 2,604 waliopata sifuri kwenye matokeo ya awali.
Kuhusu alama za CA, ofisa huyo mwandamizi wa Necta alisema kwa kawaida walimu hutuma ufaulu wa alama hizo kuanzia 70 mpaka 100 hata kwenye somo ambalo wanafunzi hawakuwahi kusoma tangu walipoanza kidato cha kwanza.
"Kwa maana hiyo, kama mtoto ana CA ya 70, ukiigawanya kwa hiyo 40 ambayo wamesema ndiyo itakuwa wastani wake, mtoto huyo tayari atakuwa na 28, hapo tayari ameshafaulu kwa hiyo mwaka huu hata watoto wote wakiamua kuacha karatasi wazi bado watakuwa na matokeo mazuri," alisema.
Wizara
Profesa Mchome hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa na wakati mwingine kukatwa.Hata alipoandikiwa ujumbe mfupi (sms), bado hakujibu.
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyanzu alisema kwa sasa wanasimamia tamko lililotolewa bungeni kuwa Serikali itawasilisha kauli yake juu ya ufafanuzi wa matumizi ya alama hizo.
Kuhusu kutozingatiwa kwa maoni ya kamati maalumu na wadau, alisema hawezi kutoa ufafanuzi wake kwa kuwa hajaona ripoti ya kamati hiyo.

No comments:

Post a Comment