Pages

Tuesday, November 5, 2013

MAGAZETI CHOCHEZI SASA KUBANWA ZAIDI


Mwanasheria Mkuu wa serikali, Frederick Werema.
SERIKALI leo inatarajiwa kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali, ambapo pamoja na mambo mengine, magazeti yanayochapisha habari za uchochezi zinazosababisha uvunjifu wa amani katika jamii, yataongezewa adhabu.
Muswada huo utawasilishwa leo bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, kuhusu sheria mbalimbali 15, ikiwamo Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 na Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza.
Vifungu vinavyofanyiwa marekebisho ni cha 36 (1) na cha 37 (1) b, ambavyo vinahusu adhabu zinazotolewa kwa magazeti yanayochapisha habari za uongo na zinazosababisha uvunjifu wa amani katika jamii.
Taarifa kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, zimeeleza kuwa Mwanasheria Mkuu alipokuwa akitoa mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho kwenye sheria hiyo, aliiambia Kamati hiyo kuwa adhabu zinazotolewa kwa magazeti yanayokiuka maadili ni ndogo, ikilinganishwa na madhara ya kosa lenyewe katika jamii.
Hivyo alipendekeza kuongeza kiwango cha adhabu ya makosa, ili kuhakikisha vyombo hivyo vinafuata utaratibu na sheria inayoviongoza.

Sheria hiyo kwa sasa kabla ya marekebisho kuletwa bungeni, kifungu cha 36 (1), kinasomeka; “mtu yeyote atakayechapisha habari za uongo, au za uzushi au kuchapisha taarifa itakayosababisha woga na kuleta uchochezi katika jamii au kuleta usumbufu, utakaondoa hali ya amani atakuwa amepatikana na hatia ya kutenda kosa na atakabiliwa na adhabu ya kulipa faini isiyozidi Sh 150,000.
Au kwenda jela miaka isiyozidi mitatu au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.” Baada ya marekebisho yanayopendekezwa, sheria hiyo inatarajiwa kuongeza adhabu ya faini hadi Sh milioni tano.
Kadhalika, kifungu cha 37 (1) b kinachohusu uchochezi kwa lengo la kusababisha vurugu na kuharibu mali, wahusika watakabiliwa na makosa ya kulipa faini ya Sh milioni tano au kwenda jela miaka mitatu au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.
Wadau

Habari za uhakika ambazo gazeti hili limeambiwa kuhusu sheria hiyo ni kwamba pamoja na kuwapo au kusikilizwa maoni na malalamiko ya wadau wa habari katika jamii, hakuna mapendekezo yaliyowasilishwa rasmi ya wadau yakiomba sheria hiyo ifanyiwe marekebisho au kubadilishwa.
“Tunafanya kazi kwa kuzingatia taratibu na kanuni, na kuna njia mbili za kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali, njia ya kwanza ni kupitia kwa Serikali yenyewe kuleta marekebisho kwenye Kamati kuhusu sheria husika kwa kuzingatia kanuni ya 80 (3),” alisema mtoa habari.
Aliongeza njia ya pili ni kwa mbunge au Kamati, kuwasilisha au kuleta muswada binafsi kwa kuzingatia kanuni ya 81(1), ambayo inaelezea marekebisho ya sheria husika na kutoa mapendekezo ya jinsi unavyotaka uwe.
Alisema kwa njia hizo mbili, yaani mbunge, Kamati au Serikali wanaweza kuwasilisha mapendekezo ya Muswada, wakitaka kufutwa kwa sheria husika na wao kutoa mapendekezo ya jinsi wanavyotaka iwe.
Mtoa habari alisema kwa kuzingatia utaratibu huo, Serikali imeleta marekebisho ya sheria hiyo, kwa kile ilichoona kinapaswa kufanyiwa marekebisho sasa.
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, mapendekezo hayo yatawasilishwa leo baada ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kushirikisha Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Idara ya Habari (Maelezo).
Alifafanua, kwamba tangazo kupitia vyombo vya habari lilitolewa kati ya Oktoba 12 hadi 14, mwaka huu, likitaarifu umma na wadau nchini kukutana na kamati hiyo, ili kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu marekebisho ya sheria mbalimbali, ikiwamo ya magazeti.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mtoa habari, pamoja na tangazo hilo, wadau wa habari hawakujitokeza kutoa maoni yao isipokuwa Idara ya Habari (Maelezo) pekee.
Wanahabari na wadau mbalimbali nchini wamekuwa wakilalamikia sheria hiyo ya magazeti wakitaka ifutiliwe mbali kwa maelezo kuwa ni kandamizi.
Sheria hiyo ndiyo imekuwa ikimruhusu Waziri mwenye dhamana na habari, kuchukua hatua kali dhidi ya gazeti linalokwenda kinyume nayo, ikiwa ni pamoja na kulifungia.
Kwa sheria hiyo, hivi sasa gazeti la kila wiki la MwanaHalisi linatumikia kifungo cha muda usiojulikana, huku Mtanzania ikitumikia kifungo cha siku 90; na hivi karibuni gazeti la Mwananchi lilimaliza kifungo chake cha wiki mbili.
Muswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa leo, huenda nao ukazua majadiliano makali miongoni mwa wabunge kutokana na kwamba huenda usizungumzie kufutwa kwa Sheria hiyo ya mwaka 1976, ambayo pia ilipata kutajwa na Tume ya Jaji Nyalali kuwa miongoni mwa sheria kandamizi.

CHANZO HABARI LEO

No comments:

Post a Comment