Timu hiyo imepeleka mashabiki zaidi ya 300 jijini
Dar es Salaam kwa lengo la kuizima Azam FC kwenye mechi ya leo Alhamisi
kwenye Uwanja wa Chamanzi.
Uongozi wa Mbeya City umekiri kwamba unatambua na
unasapoti ya mashabiki hao kwenye mechi hiyo ngumu ambayo itaamua timu
ipi itaongoza ligi mpaka mwakani kwani Azam na Mbeya City kila moja ina
pointi 26.
Timu hizo zote zipo sawa kwa kila kitu kasoro
idadi ya mabao ya kufunga tu, kwani zote zimecheza michezo 12,
zimeshinda michezo saba, zimetoa sare michezo mitano na hazijapoteza
hata mchezo mmoja na zimefungwa mabao saba kila mmoja na utofauti wao
ni Azam imefunga mabao 20 wakati Mbeya City imepachika wavuni mabao 16.
Kiongozi wa tawi kubwa la klabu hiyo lililopo
Mwanjelwa jijini Mbeya, Wille Mastala aliliambia Mwanaspoti kuwa orodha
aliyonayo inaonyesha mashabiki ni zaidi ya 300 wamejiorodhesha kwa
safari ya Dar es Salaam.
“Tumejipanga na tunauchukulia mchezo huo kwa
umuhimu mkubwa kwani tumeona jijini Mbeya timu inasapoti kubwa kutoka
kwa mashabiki, kwa nini ugenini tusiisapoti ndio tukajipanga na kuamua
kuja Dar es Salaam ili kuhakikisha Azam anakufa Alhamisi kwa mabao 2-
0,” alisema.
“Tumekodi mabasi 10 kwa ajili ya mashabiki ili
kuisapoti timu, tumefunga safari ya saa 12 kutoka Mbeya kuja Dar
kuishangilia timu,” alisema Mastala huku kocha wa timu hiyo, Juma
Mwambusi akiahidi kupambana kiume uwanjani.
Mbeya City imekuwa ikisafiri na idadi kubwa ya
mashabiki kila inapokwenda nje ya mkoa na kishindo cha shangwe kimekuwa
kikisikika zaidi inapokuwa katika uwanja wake wa Sokoine.CHANZO MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment