Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman anatarajiwa kufungua mkutano
kuhusu masuala ya adhabu mbadala wa kifungo gerezani, utakaoanza kesho
(6 Novemba, 2013) jijini Dar es Salaam.
Mkutano
huo umeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya
Huduma kwa Jamii, kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa
linalojishughulisha na Maboresho ya Sheria za Adhabu la Penal Reform International, na utafanyika katika Hoteli ya Holiday Inn, Dar es Salaam.
Lengo
la Mkutano huo ni kujadili masuala mbalimbali kuhusu kuboresha adhabu
mbadala wa kifungo gerezani na pia kupitia maazimio kuhusu matumizi ya
adhabu mbadala yaliyofikiwa katika Mkutano kama huu uliofanyika nchini
Uganda na kuzindua Mtandao unaohusu Adhabu Mbadala wa Kifungo kwa nchi
za Afrika, unaojulikana kama ‘African Alternative to Imprisonnment Network’.
Mkutano
huu wa kesho utakaoendelea hadi keshokutwa, utawashirikisha Wakuu wa
Vyombo vinavyosimamia adhabu mbadala wa kifungo kutoka nchi 10 za
Afrika. Nchi hizo ni Ethiopia, Kenya, Malawi, Rwanda, Afrika Kusini,
Sudani ya Kusini, Uganda, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.
Mkutano
huu ambao unajulikana kama Mkutano wa Uzinduzi wa Mtandao unaohusu
Adhabu Mbadala wa Kifungo kwa nchi za Afrika (Africa Alternatives to
Imprisonment Network Inaugural Meeting) utafuatiwa na Mkutano mwingine
wa Adhabu Mbadala kwa nchi za Afrika Mashariki (East Africa Alternantives to Imprisonment Conference) utaofanyika tarehe 7 hadi 8 Novemba, 2013.
Mkutano
huo, mahsusi kwa nchi za Afrika Mashariki, utawashirikisha wawakilishi
wa Idara zinazoshughulika na Adhabu Mbadala wa Kifungo (Probation and CommunityService) na
Mashirika ya Kijamii kutoka nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania.
Wafadhili na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa na washiriki wa Mkutano
wa Afrika pia wamealikwa kuhudhuria mkutano huo.
Lengo
la mkutano huo wa nchi za Afrika Mashariki ni kubadilishana uzoefu
katika kusimamia utekelezaji wa Adhabu Mbadala wa Kifungo na kuweka
mikakati ya kuboresha utekelezaji wake kwa nchi za Afrika Mashariki.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
05 NOVEMBA, 2013
No comments:
Post a Comment