MPANGO wa Taifa wa Damu Salama
Tanzania (NBTS) umevuka malengo ya ukusanyaji damu kwa asilimia 110
katika kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba 2013 ambapo jumla
ya chupa 38,552 zilikusanywa na kuvuka malengo ya chupa 35,000
zilizokuwa zikusanywe.
Ofisa Uhusiano na Masoko wa Mpango wa
Damu Salama Tanzania Bw. Rajab Mwenda alisema Kanda iliyongoza kwa
makusanyo ya damu ni Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Dar es
Salaam,Morogoro,Dodoma na Pwani ambako jumla ya chupa 13,669
zilikusanywa, Kanda inayofuatia kwa ukusanyaji damu ni Kanda ya
Kaskazini (Kilimanjaro,Arusha, Manyara, Tanga) iliyokusanya chupa 6,159.Alisema katika kipindi cha mwezi oktoba 2012 hadi Septemba 2013 takwimu zinaonyesha chupa za damu 139,676 ambayo ni sawa na asilimia 99.8 ya lengo la kukusanya chupa 140,000 ilifikiwa hata hivyo Mpango wa Taifa wa damu salama unakusanya asilimia 26 ya mahitaji ya damu kwa mwaka. Mahitaji ya damu kwa mwaka ni wastani wa chupa 400,000- 450,000.
Alisema tofauti iliyoko ya upatikanaji wa damu kwenye hospitali nchini imekuwa inafidiwa na ndugu wa wagonjwa katika kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mgonjwa.
Bw. Mwenda alisema mbalimbali ambazo zinasababisha mpango kushindwa kukusanya damu kwa 100% toka kwa wachangiaji damu wa hiari kunatoakana na uelewa mdogo katika jamii kuhusu uchangiaji damu kwa hiari kwani mfumo uliozoeleka ni ndugu wa mgonjwa ndiyo wanatoa.
Alisema nyingine ni uhamasishaji usiotosheleza toka kwa viongozi mbalimbali wa jamii, wanasiasa, viongozi wa dini, uuzwaji wa damu usio halali hospitalini jambo ambalo linawakatisha tamaa wachangia damu wa hiari, matumizi yasiyo sahihi ya damu katika hospitali na miundombinu hafifu hususan barabara duni wakati wa kukusanya na kusambaza damu.
Bw. Mwenda alisema Mpango wa Taifa wa Damu salama una wadau mbalimbali ambao hujitokeza kuchangia damu kwa hiari kama taasisi za kidini, majeshi, sehemu za kazi, mikusanyiko ya watu na wanafunzi ambao huchangia asilimia 80 ya damu hapa nchini
Alisema katika kipindi cha Novemba hadi Januari kila mwaka ni kigumu katika ukusanyaji damu kwani wadau wakuu ambao ni wanafunzi wanakuwa likizo ya mwaka hivyo Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeweka mikakati mbalimbali ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Alisema katika mikakati hiyo ni kufanya kampeni ya kuhamasisha uchangiaji damu kwa hiari katika jamii na sehemu za makanisani, minadani, stendi za mabasi, misikitini, kwenye masoko na sehemu za kazi.
Alisema wameanza kuhamasisha kambi za jeshi, makundi ya dini na ma wasiliano yamefanyika kwa jumuiya mbalimbali hapa nchini zichangie damu mfano jumuiya ya Khoja shia, Sabato na Jaula.
Pia alisema watatumia vyombo vya habari ili kuikumbusha na kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kuchangia damu na visaidie kutoa elimu na kutangaza ratiba ya ukusanyaji damu katika vituo vidogo na vikuu.
Alitoa rai kwa Watanzania kujitokeza kuchangia damu kwa hiari katika vituo vya damu salama kwa mtu yoyote mwenye afya mwanamke au mwanaume na mwenye umri kuanzia miaka 18 ajitokeze kuchangie damu.
Alisema uchangiaji wa damu kwa hiari una faida kwa mtoaji kwa vile napunguza hatari ya magonjwa ya moyo, kuwepo kwa madini chuma mengi kupita kiasi katika damu kunakodhoofisha utendaji kazi na kuchangia damu mara kwa mara hurekebisha madini chuma ya ziada katika mfumo wa damu.
Alisema faida nyingine ni upimaji wa afya pasipo gharama kwa sababu wakati unapochangia damu mtaalamu wa tiba daktari au muuguzi atapima shinikizo la damu yako, mapigo ya moyo na kukufanyia vipimo vya afya bure.
Alisema kutoa damu kunaongeza utambuzi wa kiwango cha chembe hai nyekundu na chembe na huchochea uzalishaji wa seli damu mpya na kuwaomba wanahabari kuendelea kuhamasisha na kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara kwani ni damu ya mwanadamu pekee inayotumika kumuongezea mgonjwa anayehitaji damu.
No comments:
Post a Comment