Pages

Saturday, November 23, 2013

Mtikisiko Chadema: Zitto awekwa benchi, Arfi ang'atuka, lawama zatanda



Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu Maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho ya kuwavua nyazifa Naibu Katibu Mkuu,Zitto Kabwe na  Mjumbe wa Kamati Kuu Kitila Mkumbo Katikati ni Mwanasheria wa chama hicho,Tundu Lissu na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa. PICHA | FIDELIS FELIX 
Dar es Salaam. Mgogoro ndani ya Chadema umezidi kupamba moto baada ya Kamati Kuu kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo, huku Makamu Mwenyekiti Taifa, Said Arfi akiandika barua ya kujiuzulu.
Zitto alivuliwa uongozi wa Naibu Katibu Mkuu Taifa na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati Dk Mkumbo amevuliwa ujumbe wa Kamati Kuu. Wawili hao wanatuhumiwa kukisaliti chama.
Taarifa zilisema hoja ya kukisaliti chama pia ilimkumba Arfi akidaiwa kumwezesha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita ubunge bila kupingwa, katika uchaguzi mkuu uliopita na ndiyo sababu ya kuamua kuachia ngazi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto na Dk Mkumbo, pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama. Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Kigoma Kaskazini na wadhifa mwingine kwenye Kamati ya Bunge.
Zitto azungumza
Mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Zitto aliliambia gazeti hili, “Sina cha kueleza, kikao kilikwenda vizuri na taarifa rasmi ya chama kuhusu uamuzi wa kikao itatolewa baadaye mchana (jana saa nane mchana), tusubiri Kamanda.”
Arfi ajiuzulu
Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, jana aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi ya uongozi wa chama, akisema; “…kuchoshwa na unafiki unaoendelea ndani ya chama. Napenda ifahamike pia kwangu masilahi ya wapigakura, wakazi na wananchi wa Mpanda Mjini na Wilaya ya Mpanda ni muhimu katika kuwatumikia, hivyo basi sipo tayari kuchaguliwa marafiki.
Katika barua hiyo anasema amechochwa na tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kuwa alimsadia Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita bila ya kupingwa  katika uchaguzi wa ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Kwa kipindi kirefu zimekuwepo shutuma dhidi yangu na kutiliwa shaka uhusiano wangu na Mhe Pinda Waziri Mkuu. Pamoja na kulijadili katika vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam bado yapo mashaka kwa nini alipita bila kupingwa. Huo ulikuwa uamuzi wa Wanampanda kwenu imekuwa ni tatizo, lakini hamsemi kwa nini. Majimbo mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa mlikuwa wapi na nani alaumiwe? Huu ni unafiki  wa kupindukia.
Vilevile, katika barua hiyo, Arfi anasema amechukizwa na kauli ya mwasisi wa chama hicho, aliyemtaja kwa jina moja la Mtei kuwachagulia marafiki.
“Aidha mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya Mwasisi wa chama, Mhe Mtei kutuchagulia viongozi.  Naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa mali binafsi.CHANZO  MWANAINCHI

No comments:

Post a Comment