Pages

Monday, November 4, 2013

Mursi afikishwa mahakamani


017202412_30300_99f6d.jpg
Kesi ya Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Mursi imeanza tena baada ya kuahirishwa na jaji.Washtakiwa 14 walivuruga utaratibu wa kesi kwa mayowe yao dhidi ya mahakama katika chuo cha mafunzo ya polisi Cairo.
Bendera ya Rais aliyepinduliwa madarakani Mohamed Mursi na saluti ya vidole vinne ikipeperushwa na wafuasi wake nje ya chuo cha polisi Cairo.(04.011.2013)
Haikuweza kufahamika mara moja kesi hiyo itaendelea kuahirishwa hadi muda gani leo hii Jumatatu (04.11.2013).Wapinzani wa serikali inayoungwa mkono na jeshi wanasema kesi hiyo ni sehemu ya kampeni ya kukiangamiza chama chake cha Udugu wa Kiislamu na kurudisha utawala wa mabavu.
Hadi tunaingia hewani haikuweza kufahamika kesi hiyo itaahiriswa hadi muda gani.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha kama miaka miwili hivi kwamba rais aliyepinduliwa madarakani anafikishwa mahakamani nchini Misri taifa ambalo baadhi ya watu wanahofia kwamba linarudi tena kwenye utawala wa mabavu.
Kushtakiwa kwa Mursi na wenzake 14 Waislamu wa itikadi kali kwa madai ya kuchochea mauaji ya umwagaji damu yumkini kukazusha mapambano mengine kati ya wafuasi wake na polisi.
Wanakabiliwa na mashtaka ya kuchochea ghasia zilizosababisha vifo vya takriban watu 12 katika mpambano nje ya Ikulu ya rais hapo mwezi wa Disemba baada Mursi kuwakasirisha wapinzani wake na agizo lake la kutanuwa madaraka yake.
Mamia wakusanyika nje ya mahakama
Mursi alikwenda kwenye jengo la mahakama hiyo kutoka mahala kusikojulikana kwa kutumia helikopta.Kesi hiyo inafanyika katika mahala pale pale ambapo rais wa zamani wa nchi hiyo hiyo Hosni Mubarak amekuwa akijibu mashtaka ya kushiriki katika mauaji ya waandamanaji.
Mamia ya wafuasi wa Mursi wamekusanyika nje ya jengo la mahakama kuonyesha uungaji mkono wao kwa kiongozi huyo aliyeondolewa madarakani.Bango moja lilikuwa na maadishi "Matakwa ya wananchi yamebakwa" ikimaanisha mapinduzi ya jeshi kufuatia maandamano ya umma dhidi ya utawala wa Mursi.
Mmojawapo wa mawakili wa wanaompendelea Mursi anayetagemewa kuwepo katika kesi hii leo hii amesema mashtaka yanayomkabili Mursi hayana msingi.
Amesema "Hakuna ushahidi kwamba Dakta Mursi ametenda uhalifu wa aina yoyote ile.Kesi yenye umbo la kisiasa chini ya mazingira ya mapinduzi haiwezi kufanyika kwa uwazi na kuwa ya haki."
Dhamira ya kesi yatiliwa mashaka
Mursi mwenyewe amedokeza kwamba hatambui haki ya mahakama hiyo kumshtaki na hatoteuwa timu ya wanasheria kumwakilisha.
Iwapo washtakiwa watapatikana na hatia wanaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo au kifungo cha maisha gerezani.
Chama cha Udugu wa Kiislamu kimetowa wito wa kufanyika kwa maandamano makubwa leo hii lakini ukubwa wa maandamano hayo umepunguwa kutokana na kuwepo kwa ulinzi mkubwa wa polisi.
Shirika la haki za binaadamu la kimataifa Amnesty International limesema kesi hiyo ni mtihani kwa serikali ya Misri ambayo inapaswa kuendesha kesi itayozingatia haki kwa Mursi.
Hassiba Hadj Sahraoui naibu mkurugenzi wa shirika hilo kwa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini amesema kushindwa kufanya hivyo kutazidi kutilia mashaka dhamira ya kesi hiyo.
Katika ziara ya kiongozi mwandamizi kabisa kuwahi kufanywa nchini Misri na afisa wa serikali ya Marekani tokea kupinduliwa kwa Mursi, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pia ametowa wito kwa kesi kuwa na uwazi na za haki kwa wananachi wote wa Misri.
Serikali ya Misri inakiri kwamba njia ya kuelekea demokrasia nchini Misiri imekuwa ngumu lakini mabadiliko sahihi ya kisiasa yatafanyika.
Mwandishi:Mohamed Dahman/ Reuters

No comments:

Post a Comment