Ndege
mbili za kijeshi za Marekani zimepita katika anga za China katika eneo
linalozozaniwa kati ya China na Japan la visiwani bila ya kuiarifu na
kupuuza agizo la China kutaka kuarifiwa mapema kutumika kwa anga zake.
Wataalamu
wa masuala ya kidiplomasia wanaona ukiukaji huo wa masharti ya China
kuhusu kutumika kwa anga zake kutoka kwa Japan na washirika wake
Marekani kutachochea hata zaidi mzozo ulioko wa kusimamia eneo la visiwa
kati ya Beijing na Tokyo na kuifanya China kuchukua hata hatua zaidi
kusisitiza ubabe wake.
Mwishoni
mwa wiki iliyopita China ilichapisha kanuni mpya za kuanzisha eneo
maalum la ulinzi wa anga katika eneo lenye mzozo wa maji katika bahari
ya China Mashariki na kutangaza kuwa ndege zinazopita katika eneo hilo
la bahari, sharti zitii maagizo yake.
Ndege
zitakazokuwa zikiingia katika eneo hilo zitatakiwa kutoa taarifa za
awali kabla ya kupita katika eneo hilo na kudumisha mawasiliano kwa
kujibu maswali yatakayohitajika kutoka kwa waongozaji ndege.
Chanzo cha mzozo ni visiwa
Eneo
hilo la ulinzi linahusisha visiwa vya Senkaku na Diaoyu ambavyo vimekuwa
chachu ya kuongezeka kwa mzozo baina ya mataifa hayo mawili. China
imesema itadhibiti anga na visiwa vyake mashariki mwa nchi hiyo na
kuonya kuwa itachukua hatua za dharura za kujilinda dhidi ya ndege
yoyote itakayofeli kuzingatia sheria zake.
Chombo cha majini cha Kijeshi cha China kikishika doria
Profesa
Sun Zhe wa chuo kikuu cha Tsinghua mjini Beijing amesema iwapo Marekani
itaendesha ndege zake mara mbili tatu kama ilivyofanya wakati huu, basi
itailazimu China kuchukua hatua ambazo hazitakuwa za maneno matupu tu.
Wizara
ya ulinzi ya China imesema ilifuatilia nyendo zote za ndege hizo za
kijeshi za Marekani jana lakini msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani
amesema ndege hizo hazikufuatiliwa wala hazikupokea mawasiliano yoyote
kutoka China.
Shirika
la ndege la Japan, ANA, limesema kufuatia ombi kutoka kwa serikali
yake, limesitisha kutoa taarifa zozote za mipango ya safari za ndege
zake kwa maafisa wa China na haijashuhudia matatizo yoyote wakati
ikipita katika kanda hiyo na kuongeza hakuna kitisho kwa usalama wa
abiria wake.
Japan yajiimarisha kukabiliana na vitisho
Hatua
hiyo ya China pia inaonekana kutoa fursa kwa waziri mkuu wa Japan,
Shinzo Abe, kupata mashiko ya hoja yake ya kupewa nguvu zaidi za
kuboresha jeshi lake ili kukabiliana na vitisho vyovyote kutoka nje.
Rais wa Marekani Barrack Obama na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe
Japan
leo imeunda baraza la kitaifa la usalama ambalo limeidhinishwa na bunge
linalompa waziri mkuu mamlaka zaidi kuhusu masuala ya kiusalama na sera
za kigeni na ulinzi hatua inayoonekana kutokana na mzozo huu uliozuliwa
upya na China.
Marekani
ambayo ina mamia ya ndege za kijeshi katika kanda hiyo imesema haina
nia ya kuzingatia kanuni mpya zilizowekwa na China huku Japan ikizitaja
hatari na zisizokubalika. Taiwan na Korea Kusini ambazo pia ni washirika
wa Marekani katika kanda hiyo pia zimetupilia mbali masharti hayo ya
China.
Hata
Australia imejiingiza katika mzozo huo kwa kumuita balozi wa China
nchini humo kuelezea wasiwasi wao kuhusu maagizo hayo ya kudhibiti anga
yake.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Ap
Mhariri: Josephat Charo
No comments:
Post a Comment