Pages

Tuesday, November 5, 2013

Polisi sasa wanasa mtekaji mkuu Moshi



Moshi. Polisi imemtia mbaroni mtuhumiwa muhimu katika tukio la mwanamke mmoja mjini Moshi aliyetekwa nyara na watu wasiojulikana na kwenda kutelekezwa jijini Dar es Salaam.
Mwanamke huyo alichukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni askari wa upelelezi kutoka Dar es Salaam na kwamba, walikuwa wametumwa kumkamata kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema mtuhumiwa huyo muhimu (jina tunalo) alikamatwa Dar es Salaam na kusafirishwa hadi Moshi mwishoni mwa wiki iliyopita. Tukio hilo lilitokea Oktoba 13 mwaka huu eneo la Soweto NHC, watu hao walimchukua mwanamke huyo, Asha Amini hadi Dar es Salaam na kumpora Dola 11,000 za Marekani.
Boaz alisema aliyetoa taarifa hizo polisi, ni Jerome Mushi na alijitambulisha kuwa ni mume wa mwanamke huyo.
“Aliporudi nyumbani (Mushi) hakumkuta mkewe akaambiwa amekamatwa na polisi na amepelekwa Kituo Kikuu akaamua kwenda hadi kituoni wakamwambia hakuna tukio kama hilo,” alisema Boaz.
Kamanda Boaz alisema jalada la uchunguzi lilifunguliwa na siku hiyo hiyo watu walioondoka na mwanamke huyo, walimpigia simu mumewe wakitaka walipwe Sh2 milioni.
Hata hivyo, Boaz alisema watu hao walimwachia huru mwanamke huyo eneo la Bunju Dar es Salaam bila kumdhuru na kumpa Sh50,000 za nauli ya kumfikisha katikati ya jiji.
Kwa upande wake, Jerome Mushi alisema waliomchukua mkewe walikuwa na bastola moja, pingu mbili na redio moja ya upepo na walichukua dola 11,000 za Marekani.CHANZO MWANAINCHI

No comments:

Post a Comment