Pages

Monday, November 4, 2013

SUGU KUKUSANYA SAINI ZA WABUNGE KUZUIA MAGAZETI YASIFUNGIWE

sugu_2dc95.jpg
NA BENJAMIN MASESE, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), leo anatarajia kuanza kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kumuondolea dhamana waziri anayeshughulikia habari, kutumia kifungu cha 25 cha sheria ya mwaka 1976 ya kuyafungia magazeti.
Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara hiyo, alisema baada ya kukusanya saini hizo atawasilisha bungeni hati ya haraka ya muswada binafsi wa sheria ya marekebisho ya sheria ya magazeti ya 1976, kwa lengo la kurekebisha kifungu cha 25 kinachotumiwa vibaya na waziri kuvifungia vyombo vya habari kutochapisha habari.
Akizungumza na RAI Jumatatu jana alisema kutimiza masharti ya kanuni ya uwasilishaji wa hati binafsi, amewaomba wabunge kutia saini kwa lengo la kumuunga mkono ili vyombo vya habari viweze kufanya kazi yake vizuri.
Alisema ameamua kufanya hivyo kwa kuzingatia taratibu zote za muswada za sheria utaolazimika kuchapwa kwanza katika gazeti la Serikali.
"Kwa vyovyote vile Serikali itatumia kisingizio cha kesi iliyofunguliwa na Hali Halisi Publishers ya mwaka 2009, ambayo ilifunguliwa baada ya Gazeti la Mwanahalisi kufungiwa.
"Lakini hadi leo kesi haijasikilizwa ambapo Serikali inafanya makusudi kuchelewesha kusikilizwa kwa kesi hiyo ndani ikiwa sasa ni miaka minne na sheria hiyo imeendelea kuyafungia magazeti mengine.
"Hivyo basi kukwepa kikwazo hicho, nitawasilisha muswada wa dharura wa kufanya marekebisho, sio kufuta bali kumwondolea waziri mwenye dhamana mamlaka ya kufungia, kusitisha kuchapisha gazeti lolote au magazeti yoyote.
"Serikali haitaweza kutumia kisingizio cha kesi iliyo mahakamani kufanya marekebisho ya sheria hiyo, kwa sababu pamoja na kesi kuwapo mahakamani, tayari imeshasoma kwa mara ya kwanza bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba tatu wa 2013 ambao katika vifungu vya 40 na 41 inakusudia kufanyia marekebisho vifungu vya 36(1) na 37 (1) (b).
"Kwa ajili ya kuongeza faini kwa magazeti kutoka Sh 150,000 hadi Sh milioni tano kwa makosa ya kashfa," alisema.
Hivi karibuni, Serikali imeyafungia magazeti mawili likiwamo la MWANANCHI kwa siku 14 na MTANZANIA siku 90 ambalo hadi sasa linaendelea kutumikia kifungo hicho.
Serikali ilitumia sheria hiyo ambayo inampa dhamana waziri husika kuchukua hatua dhidi ya gazeti husika lililochapisha habari ya kashfa.

No comments:

Post a Comment