Pages

Tuesday, November 5, 2013

TAMKO LA HAKIELIMU KUHUSU UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU



4 NOVEMBA 2013.

Hivi karibuni serikali imetoa tamko kuhusu mfumo mpya wa upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi na ufaulu. HakiElimu na wadau wake imetafakari tamko hilo na kutoa maoni ya yafuatayo:

1. Hatujatambua lengo la serikali kuleta mabadiliko haya; hasa ikikumbukwa kuwa Tume ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mh. Mizengo Pinda haijawahi kuweka bayana taarifa yake kuhusu sababu za wanafunzi kutofaulu vizuri katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne. Wajumbe wa Tume hiyo wamekuwa wakitoa dondoo fupi fupi za matokeo ya kazi yao-kama vile Bungeni na katika hadhira nyingine za kitaifa; bila kutoa ripoti yenyewe. Je, kwa mabadiliko haya,wizara inataka kuwaaminisha Watanzania kwamba alama zilivyokuwa zimepangiliwa hapo awali,ndiyo sababu kuu ya wanafunzi kutofaulu vizuri?

2. Wizara imeeleza kwenye tamko lake kwamba imeshirikisha wadau mbalimbali katika kufikia uamuzi huo. Hata hivyo, katika orodha ya wadau walioshirikishwa inaonekana bayana kuwa asasi za utetezi hazikupewa nafasi. Baada ya kufanya mawasiliano na baadhi ya wadau wanaodaiwa kushiriki,wenyewe wamekiri kuwa ingawa walishiriki mawazo yao hayakuzingatiwa na hawakukubaliana kuhusu kushusha alama za ufaulu kufikia 20 kati ya 100.

3. Mpangilio wa alama zitakazotumika kuanzia mwaka huu unaleta tafsiri ya ndani kuhusu nia ya wizara kubadilisha alama hizo. Tafsiri hiyo ni kulazimisha kuona kwamba wanafunzi wachache zaidi wanapata daraja la 5 (ambalo limeanzishwa badala ya daraja sifuri); kukiwa na uwezekano wa kupunguza wanafunzi wanaopata daraja hili kwa asilimia 2.2% ukilinganisha na utaratibu uliotumika kwa matokeo ya mwaka 2012. Mpangilio huo mpya una uwezekano wa kuongeza kundi la wanafunzi wanaopata daraja la tatu na la nne kwa asilimia 12.1% kuliko utaratibu uliotumika mwaka 2012. Hata hivyo, alama hizo mpya zinaweza kupunguza uwezekano wa kupata daraja la kwanza na la pili kwa asilimia 11.9%. Serikali na wadau wengine wa elimu wanatambua bayana kuwa njia kuu ya kuboresha elimu na matokeo katika mitihani ni kuboresha utaratibu wa utoaji wa elimu. Kwa nini serikali, hasa katika kipindi hiki inataka kuona matokeo mazuri bila kuwekeza kwenye mipango ya kuboresha mfumo na utaratibu wa utoaji wa elimu? HakiElimu inatafsiri uamuzi huo wa serikali kama ni kukwepa ukweli na utaalamu; na badala yake serikali inatafuta njia ya mkato ya kuwafurahisha wazazi na wananchi ili wapunguze kelele.

4. Serikali imekubali kutumia asilimia 40 kutoka kwenye Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment, CA), ili ziunganishwe na alama 60 za mtihani wa mwisho. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa alama hizo zilikuwa zinachakachuliwa huko shuleni, na hata Baraza la Mitihani Tanzania mwaka huu walikiri hilo kutokea. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itatumia njia gani kuhakikisha kuwa zinapatikana alama sahihi toka shuleni zinazoendana na uwezo wa mwanafunzi? Je, kwa kiasi gani walimu wameandaliwa na kujengewa mazingira mazuri ya kufanikisha zoezi hili? Hata hivyo, serikali inapaswa pia kuwaeleza watanzania uzoefu wa nchi nyingine za Afrika katika matumizi ya alama za CA; wengine wanatumia asilimia ngapi? Ni muhimu kuwa na ushahidi kuwa kiwango cha CA tutakachokitumia kitaboresha utaratibu wa kutathmini wanafunzi; na kuwatendea haki badala ya kuwaghiribu au kuwaumiza.

5. HakiElimu inasikitika kuona wizara inalazimisha kila mwanafunzi atakayefanya mtihani wa kidato cha nne au cha sita awe amefaulu. Hiyo inathibitishwa na tafsiri ya alama ambazo zitatumika zinazoonesha kwamba kuanzia atakayepata alama sifuri mpaka mia moja atakuwa amefaulu kwa namna fulani. Kwa mfano, hata atakayepata alama kuanzia 0 mpaka 19 katika somo fulani atahesabiwa kuwa amefaulu, japo katika kiwango kisichoridhisha. Kwa nini wizara inakosa ujasiri wa kukubali kuwa mwanafunzi atakayepata chini ya alama fulani ahesabiwe kuwa hakufaulu?

6. Kwa upangaji huo mpya wa alama za ufaulu, Tanzania itakuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kwa kuwa na kiwango cha chini kabisa cha ufaulu katika elimu ya sekondari na kuna hatari kwamba kushushwa kwa alama za ufaulu kutapunguza ama kuondoa hamasa ya wanafunzi kusoma kwa bidii, kwa kuamini kuwa hawatafeli na cheti watapata tu. Kama wadau wote tunakubaliana kuwa nia ya kutoa elimu ni kuandaa Watanzania ambao watakuwa na maarifa na uwezo wa kushindana na wengine wanaosoma katika nchi nyingine Afrika.

7. HakiElimu pia inasikitika kuona kuwa wizara inapotosha malengo ya “Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now-BRN)” kwa kutafuta njia za mkato. BRN imeeleza bayana kuwa kati ya mikakati itakayotumika kupata Matokeo Makubwa katika elimu ni kuboresha mchakato wa kufundisha na kujifunza shuleni na kuboresha utaratibu wa utoaji wa elimu kwa kuweka bayana majukumu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya TAMISEMI. Wizara iwaambie Watanzania kuwa kwa kiasi gani upangaji huu wa alama utasaidia kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa maana ya kumjengengea mwalimu uwezo, mazingira mazuri na hamasa ya kufundisha na pia kutengeneza mazingira mazuri ya mwanafunzi kujifunza. Katika haya, je, ni kweli kwamba huu upangaji upya wa madaraja ni kipaumbele chetu namba moja? Si busara kushughulikia mpangilio wa alama na madaraja kwanza wakati mchakato wa kuboresha mfumo wa elimu ili kupata hayo matokeo mazuri bado uko chini. Kitendo hicho ni kukurupuka na kuruka hatua muhimu zinazoweza kuboresha elimu.

8. HakiElimu inawatahadharisha Watanzania, wakiwemo wazazi, wanafunzi na vijana wenye nia ya kurudia mitihani ili wapate vyeti; na serikali yenyewe kuzingatia ukweli kwamba: Elimu ni uwezo, SIYO cheti. Jitihada za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonesha wazi kuwa nia ni kuona matokeo mazuri hata kama matokeo hayo hayataendana na uwezo walio nao wanafunzi. Katika kutengeneza raslimali watu ya kutosha, Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine haina namna ya kukwepa kuhakikisha kwamba mfumo wa elimu unaandaa vijana au wananchi wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili wao wenyewe, jamii na Taifa kwa ujumla; pia kuwa na wananchi ambao watakuwa na ujasiri, tija na ubunifu, katika uzalishaji katika shughuli na fursa mbalimbali watakazozipata au kuzitafuta. Hali hii haipatikani kwa kuhangaika na alama za ufaulu kama kipaumbele. Tunahitaji kuhangaika na mfumo wa utoaji elimu utakaotusaidia kuleta mapinduzi ya kweli ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

HakiElimu inaishauri Serikali kusitisha matumizi ya alama na madaraja haya mapya. Irudi kwa wadau na ushahidi kuhusu uamuzi huu; huku ikitoa nafasi ya kuchukua maoni ambayo yanaweza kuboresha mfumo wa upimaji wa wanafunzi. Wakati zoezi hilo linaendelea, HakiElimu inaisisitiza Serikali kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali na mipango iliyopo kushughulikia dosari na changamoto zinazorudisha nyuma elimu yetu, hasa zile zinazokwamisha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
Tamko hili limesainiwa na,

Elizabeth Missokia Mkurugenzi Mtendaji, HakiElimu

No comments:

Post a Comment