Watu saba wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa vibaya baada ya magari mawili ya abiria yanayofanya safari zake kutoka jijini Tanga kwenda wilayani Korogwe kugongana uso kwa uso katika kijiji cha Chang'ombe kilichopo katika barabara kuu inayounganisha mikoa ya Tanga kwenda Kilimanjaro.
Waliofariki katika ajali hiyo wametambulika kuwa ni
Ramadhani Waziri kondakta wa Concorde, Jumanne Abdalla dereva wa basi
hilo dogo, Nuia Mohamed abiria,Shamina Mbago abiria,William Samwel
abiria,Martin Msembo na mmoja ambaye hadi sasa mwili wake
haujatambuliwa.
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wakizungumza na
ITV katika hospitali teule ya wilaya ya Korogwe ya magunga ambapo
wamelazwa kwa ajili ya matibabu wamesema madereva wa magari yote mawili
ya kampuni ya mabasi ya ''Zamoyoni na concorde''walikuwa katika mwendo
kasi hivyo wakati wakiwa katika harakati za kukwepa mbuzi huku wengine
wakidai kuwa ni mbwa na mwanae waliokuwa wakivuka barabara ndipo
walipogongana uso kwa uso na kusababisha watu watano kufa papo hapo.
Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Korogwe
Dr. Rashid Said amesema katika ajali hiyo wamepokea majeruhi 24 na miili
mitano ya waliofariki isipokuwa baadae katika majeruhi wanne waliokuwa
na majeraha makubwa sehemu za kichwani wawili kati yao walifariki na
kuongeza idadi kufikia saba.
Naye kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga Costantine
massawe ametoa wito kwa madereva kuheshimu maisha ya abiria badala ya
kukwepa mbuzi hivyo amewataka wakazi wanaofuga mifugo yao pembeni mwa
barabara kufungia mifugo ili isiweze kusababisha ajali barabarani.
No comments:
Post a Comment