KATIBU wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Dar es Salaam,
Henry Kilewo, jana alihojiwa kwa muda na maofisa wa Jeshi la Polisi
kutoka makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam, akihusishwa
kutishiwa maisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA).
Kilewo
aliwasili katika makao makuu ya jeshi hilo jana majira ya saa 06:03
mchana, akiwa ameongozana na wanasheria wawili pamoja na Diwani wa
Ubungo, Boniface Jacob, huku waandishi wa habari waliopiga kambi katika
eneo hilo la makao makuu ya Polisi kwa ajili ya kufuatilia
kinachoendelea wakilazimishwa kuondoka.
Baada ya
kuwasili, Kilewo na wanasheria wake walifika katika eneo la mapokezi
na kujitambulisha, ambapo askari aliyekuwa na cheo cha sajenti
aliwaelekeza idadi ya watu wanaoruhusiwa kuingia katika chumba cha
mahojiano kuwa ni Kilewo mwenyewe na mwanasheria wake.
Hata
hivyo maelekezo hayo ya polisi yalipingwa na wanasheria wa Kilewo, John
Malya, ambaye alishinikiza waingie wote kwa ajili ya kusikiliza kile
alichoitiwa mteja wao, hali iliyozua mabishano ya muda kabla ya baadhi
ya maofisa wa polisi kuridhia matakwa ya wanasheria hao kuingia wote kwa
ajili ya mahojiano.
Mara
baada ya kuingia ndani, Kilewo na wanasheria wake walikaa kwa zaidi ya
saa mbili kabla ya kutoka, ambapo mwanasheria wake, Malya, alizungumza
na waandishi wa habari na kuelezea kile kilichosababisha mteja wake
kufika katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.
Malya
alisema mteja wake alipata wito wa polisi kupitia simu ya kiganjani kuwa
anahitajika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano huku
akiwa hajafafanuliwa ni mahojiano ya namna gani na yanahusu jambo lipi.
Alisema baada ya wito huo wa njia ya simu walifika jana kuitikia wito, huku wakitaka kujua kilichosababisha mteja wao kuitwa.
“Kiutaratibu
hawakufuata sheria, kwa kuwa hawakutoa hati ya wito au ya kukamatwa na
zaidi hakuna mtu aliyefungua mashitaka dhidi ya mteja wangu,” alisema.
Aliongeza
kuwa walipofika polisi waligundua kuwa mtu aliyefungua malalamiko ya
kutishiwa maisha na mteja wake kutakiwa kutoa maelezo katika fomu ya
onyo ya Jeshi la Polisi ni Zitto Kabwe.
Alisema
hali ya kutakiwa kuweka maelezo katika fomu ya onyo ilizua mjadala baada
ya kutaka kujua kosa linalosababisha mteja wake kuhojiwa.
“Tuliwaambia
wabadilishe fomu ya maelezo isiwe ya onyo, itumike ile ya ripoti nao
wakakataa, tukakubaliana pale panapoandikwa kosa la mhusika papigwe
mstari, kwa kuwa hawakutuambia mteja wetu anashitakiwa kwa kosa lipi,”
alisema Malya.
Alisema
maelezo ya polisi waliyoyatoa kwao ni kuwa wanafanya uchunguzi juu ya
taarifa zilizoandikwa katika gazeti la Majira juu ya Zitto Kabwe
kutishiwa maisha na kwamba mteja wake alitoa maelezo na kisha
kujidhamini mwenyewe.
Kilewo atoa kauli
Akizungumza baada
ya kutoka katika mahojiano, Kilewo alisema Jeshi la Polisi linapaswa
kubadilika na kufuatilia masuala ya msingi na liache kujiingiza kwenye
masuala ya siasa.
Alisema
ni jambo la kusikitisha kuona polisi wanakuwa wa kwanza kuwafuata
wanasiasa huku wakishindwa kuainisha hatua waliyofikia katika matukio ya
kutekwa na kisha kujeruhiwa kwa mwandishi wa habari, Absalom Kibanda,
tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Stephen Ulimboka na wengine.
“Nchi
inakabiliwa na mambo makubwa, kuna uhalifu unaotishia maisha ya
Watanzania, badala ya polisi kuhangaika na hivyo wao wanageuka kuwa
wanasiasa,” alisema Kilewo.
Kwa
upande wake Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP Advera Senso, alikanusha
kuwa wito wa katibu huyo wa CHADEMA hautokani na malalamiko ya Zitto,
bali ni utaratibu wa kawaida kwao kumuita mtu yeyote na kuongea naye
pale wanapoona kuna haja ya kufanya hivyo.
Kuhusu
waandishi kufukuzwa katika eneo la polisi, Senso alisema polisi haikuwa
na haja ya kuita vyombo vya habari katika tukio hilo, na kama mhusika
aliviita, waandishi wa habari walipaswa waende katika ofisi yake.
No comments:
Post a Comment