Johannesburg. Afrika
Kusini, jana ilitawaliwa na ibada na maombi yaliyofanyika katika
makanisa mbalimbali kuliombea taifa, baada ya kifo cha Rais wa Kwanza
mzalendo, Nelson Mandela.
Rais
Jacob Zuma alikuwa miongoni mwa waumini wa Kanisa la Bryanston
Methodist, Johannesburg katika ibada ambayo pia ilihudhuriwa na mtalaka
wa Mandela, Winnie Madikizela pamoja na mjukuu mkubwa, Mandla.
Ibada
za aina hiyo ziliendeshwa kila kona ya nchi, zikiwaweka pamoja Waafika
Kusini ambao waliitikia wito wa Rais Zuma wa kuitumia Jumapili kuliombea
taifa hilo.
Nyimbo
za dini zilisikika katika kumbi za ibada na makanisa, ambako viongozi
wa Serikali wakiwamo Naibu Rais wa Afrika Kusini, Kgalema Motlante na
Rais Mstaafu, Thabo Mbeki walikuwa miongoni mwa waliopangiwa kushiriki
katika ibada hizo.
Katika
Kanisa la Baptist, baadhi ya waumini wakiwa katika mavazi rasmi
walionekana wakiimba na kucheza, kabla ya Rais Zuma kupewa nafasi ya
kuzungumza.
“Kwa
nchi yetu, kifo cha Baba Madiba ni hasara ya aina yake. Waafrika Kusini
tunapaswa kuomba tukikumbuka mambo mema ya kiukombozi na uhuru, amani,
msamaha, haki na kujali ambayo Mandela aliyapigania na kuyasimamia,”
alisema Zuma.
Kwa
upande mwingine, mamia ya wafuasi wa Chama cha African National
Congress (ANC), walifurika katika Ukumbi wa Benki ya Standard,
Johannesburg kushiriki katika maombi, wakiitikia wito wa Rais Zuma.
Mwandishi
wetu alishuhudia makada wa chama hicho wakiwa katika mavazi rasmi,
wakicheza muziki wa Injili na baadaye wakishiriki maombi yaliyowahusisha
waumini wa madhehebu ya Kikristo, Kiislamu, Kihindu, Kiyahudi, Bahai na
wale wanaoamini katika imani za jadi.
Qunu kimya
Wakati
nyimbo na ngoma zikichezwa kwa ajili ya kusifu kazi alizofanya Mandela,
katika Kijiji alichokulia Qunu, eneo la Mthatha kuliripotiwa kuwa kimya
huku wakazi wake wakikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu
kifo cha Mandela.
Wanakijiji
hao wameamua kukaa nyumbani wakiomboleza na inaaminika kwamba wengi
hawaamini kilichotokea na pengine wanasubiri kushuhudia mwili wa
kiongozi huyo utakapofikishwa huko Jumamosi kwa ajili ya mazishi
yatakayofanyika Jumapili.
Hata
hivyo, hali ni tofauti katika Kijiji cha Mvezo alikozaliwa Mandela,
ambako tangu Ijumaa, wakazi wake wamekuwa wakiamka asubuhi na kushiriki
katika ibada na maombi hadi adhuhuri, kisha kurejea tena jioni.
Kitukuu
wa Mandela, Mambui alisema hali katika kijiji hicho kilichopo umbali wa
Kilometa 25 tu kutoka Qunu ni ya huzuni na kwamba watu wake wamekuwa
wakiomboleza kwa kulia machozi hasa wanapokuwa katika nyumba zao.
“Ni
machozi ya huzuni na maumivu moyoni, siyo machozi ya furaha hata
kidogo,” alisema Mambui alipokuwa akihojiwa moja kwa moja na Kituo cha
Televisheni cha Afrika Kusini (SABC), jana asubuhi.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment