skip to main |
skip to sidebar
KIONGOZI WA MADAKTARI NA DAKTARI BINGWA DK RODRICK KABANGILA AJIUNGA NA CHADEMA
Ndugu waandishi
Ndugu waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla, kwanza kabisa napenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kufikisha miaka mitatu
ya kuwatumikia Madaktari na Watanzania kwa ujumla kwa vile nimekuwa
kiongozi wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT) kwanza kama Katibu Mkuu
wa Chama hicho kwa miaka miwili na baadae Makamu wa Rais wa Chama hicho.
Kwa kupitia nafasi hizo za MAT nimeweza kuwa Makamu wa Rais wa
Shirikisho la Vyama vya Kitaaluma vya Afya ambapo shirikisho hilo
linajumuisha vyama vyote vya kitaaluma katika sekta ya afya. Nafasi
nyingine muhimu ya kujivunia kuwatumikia Watanzania kitaaluma ni pamoja
na kuwa katibu mkuu wa kwanza wa Chama Cha Wafanyakazi Madaktari na
Wafamasia Tanzania (TMDPWU) nikiwa mwanzilishi na kaimu katika nafasi
hiyo.
Ndugu waandishi
Katika kipindi cha uongozi wangu
nikishirikiana na wenzangu tumejitahidi kushiriki katika uboreshwaji
wahuduma za afya Tanzania, na yafuatayo ni mfano;
1. Kushiriki
katika kupitia Rasimu ya Sheria ya Madaktari ambayo itawezesha madaktari
kufanya kazi kwa weledi zaidi na hivyo kupunguza makosa ya kitaaluma
wakati wa utoaji wahuduma za afya. Rasimu hii iko katika hatua za mwisho
za kwenda bungeni.
2. Kuandaa rasimu na kusajili chama cha
Wafanyakazi Madaktari na Wafamasia Tanzania ambacho kitajikita zaidi
katika kudai maslahi huku kikiacha MAT kifanye kazi ya kuboresha
taaluma. Chama hiki tayari kinaendelea kushamiri katika vituo vya kazi
vya madaktari.
3. Kudai mazingira bora ya kazi katika sekta ya afya
ikihusisha upatikanaji wa vifaa tiba na madawa kwa manufaa ya kuboresha
hudumaza afya.
4. Kwa kushirikiana na SIKIKA kufanya utafiti
uliowezesha kujua upungufu mkubwa wa madaktari katika utoaji wa huduma
za afya. Utafiti huu utaiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi katika
kushughulikia suala la Rasilimali watu katika afya.
Pamoja na
haya yote mazuri niliyohusika katika kuongoza Madaktari na kuwa na moyo
wa kuendelea kufanya hivyo, bado kuna mambo mengi hayaendi vizuri ambayo
ni ya kimfumo katika serikali hii ya CCM ambayo yanaendelea kudidimiza
huduma za afya. Mifano mizuri katika hili ni urasimu usio na maana
katika usambazaji wa madawa na vifaa tiba, kutojali wataalamu, ufisadi
na uzembe kauanzia wizarani, taasisi zake mfano Bohari la dawa mpaka
katika vituo vya afya.
Ni kutokana na sababu hii inakuwa ngumu
kwa vyama vya kitaaluma kuweza kuletama badiliko makubwa katika sekta
hii na hivyo kuendelea kwa huduma duni za afya.
Naamini kuwa ili
kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya katika jamii hii ya
kitanzania kuna haja ya kubadilisha mfumo huu wa afya uliopo kwa kupata
sera madhabuti zenye kujali Mtanzania maskini ambaye kwa kiasi kikubwa
hawezi kumudu gharama za afya zinazopanda kila siku. Kwa hiyo mchango wa
kisiasa ili kuwezesha haya unahitajika ili kubadilisha sekta hii ya
afya Tanzania.
Ndugu waandishi
Ni kwa nia hii nzuri niliyo
nayo na niliyoonyesha ya kuboresha sekta ya afya nchini ninafurahi
kusema kuwa sasa ninahamishia rasmi nguvu zangu katika Chama cha siasa
na hiki si kingine ni CHADEMA ambacho kimejipambanua kuwa chama cha watu
kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Na kwa vile tayari nimeaminiwa
kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya ZiwaMagharibiwa
CHADEMA, nitatoa mchango wangu katika chama hicho ambacho nina hakika
kitaweza kufikisha mazuri katika vyombo husika vya kimaamuzi mfano ni
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, halmashauri n.k.
Hivyo basi kwa kupitia sababu hii ya kuwa Kada rasmi wa CHADEMA bila
kushurutishwa na kwa hiari yangu nang’atuka nafasi zangu zote za
kuongoza Madaktari na watumishi wengine wa afya na tayari nimepata
Baraka ya Halmashari kuu ya MAT ya kufanya hivyo kupitia kwa Rais wa
Chama hicho;
Ndugu waandishi,
Nimeamua kufanya maamuzi haya ili
i) Kuondoa mgongano wa kimaslahi (conflicts of interests) kati ya Vyama ninavyoongooza, Madaktari, mimi mwenyewe na CHADEMA.
ii) Kuweza kuchangia kwa karibu zaidi katika Chama hiki kwa mawazo
yangu ya kitaaluma ambayo nina hakika yatafanyiwa kazi na kuwa na
manufaa zaidi katika uboreshaji wa sekta hii hasa wakati huu ambapo
chama tayari kinaendelea kuandaa sera zake mbalimbali ikiwemo sera ya
afya.
iii) Nikiwa kama msomi napenda kukiri waziwazi kuwa
nitajishughulisha bila kificho katika kutoa mawazo na utaalamu wangu
CHADEMA ili tuweze kwa pamoja kuwa na sera nzuri na kuboresha huduma za
afya Tanzania.
iv) Kuwakumbusha watumishi wote wenye taaluma
mbalimbali kuwa kushiriki katika harakati za kisiasa ili kuiondoa CCM si
kosa la jinai kama ambavyo inataka kuaminishwa, na hii inajionyesha
hata katika vifungu vya kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa
umma;
• 5 (1) – Kinatoa haki ya kidemokrasia ya kuwa mwanachama wa Chama chochote.
• 5 (2) – Kushiriki masuala ya siasa lakini usionyeshe upendeleo wa kisiasa
• 5 (3) (a) – Usijuhusishe na siasa saa za kazi au mahala pa kazi
Ndugu waandishi
Napenda kuwashukuru Madaktari na watumishi wengine wa afya walioniamini
na kunipa uongozi katika kipindi chote hiki na kuwa mimi bado ni
mtaaluma na nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Vyama hivyo. Pia
napenda kuupongeza nakuushukuru uongozi imara wa CHADEMA kwa kuniamini
na kunipa nafasi ya mimi kushiriki katika mapambano haya ya ukombozi.
Mwisho kabisa, Napenda kuwasihi wataalamu wote wa chi hii kutokuwa
waoga katika kujihusisha na mageuzi ya kiuchumi na kijamii ya nchi hii
yanayoendelea na kwamba waache kulalamika tu bali wachukue hatua. Nchi
hii ni yetu sote na sote tushiriki
kuijenga.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
Dr. Rodrick Kabangila - Daktari bingwa wa Magonjwa ya Tiba, tafiti za huduma za afya na epidemiolojia
Mhadhiri Mwandamizi – CUHAS - Bugando
Makamu Mwenyekiti – CHADEMA Kanda yaziwa Magharibi
No comments:
Post a Comment