Arusha. Dalili
za amani na usalama Mkoa wa Arusha zimeanza kuonekana mapema baada ya
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwakutanisha viongozi mbalimbali
vya vyama vya siasa, dini na wabunge wa vyama tofauti kujadili
changamoto kuu katika suala la amani.
Katika
kipindi cha hivi karibuni, Arusha umekumbwa na vurugu za hapa na pale
hali iliyosababisha baadhi kupoteza maisha katika matukio tofauti
likiwamo bomu lililolipuka katika mkutano wa kuhitimisha kampeni za
uchaguzi mdogo wa Chadema eneo la Soweto na kuua watu 4 na wengine zaidi
ya 50 kujeruhiwa.
Katika
mkutano uliofanyika jana, ilitolewa kauli moja ya kuitisha mkutano
mkubwa wa amani utakaofanyika Desemba 6 mwaka huu katika Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid.
Mkutano
huo utawashirikisha wafuasi kutoka vyama mbalimbali vya siasa, dini
tofauti na wale wasio na vyama ambapo katika makubaliano yaliyoafikiwa
kuelekea katika mkutano huo mojawapo ni washiriki kutovaa sare za vyama
vyao.
Akifungua
mkutano huo, Msajili Francis Mutungi alisema kuwa lengo la ofisi yake
kuwakutanisha wadau hao ni kutafuta amani mkoani Arusha.
Alisema
kuwa hakuna mtu anayestahili kuipuuza amani katika Mkoa wa Arusha,
ambao unachangia pato kubwa la taifa hususan katika sekta ya utalii.
Mutungi
alisema wakazi wa Arusha wanapaswa kuzingatia amani katikati ya udini
na ukabila. “Ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anasaidia kuleta
amani katika eneo lake kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na jeshi
la polisi,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema kuwa changamoto kubwa katika mkoa wake ni suala la amani.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment