Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick SumayeMsemo wa sheria ni msumeno, umedhihirika
sasa kwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye anataka sheria
iliyohalalisha matumizi ya takrima kwenye uchaguzi ifutwe.
Sheria
hiyo iliyopitishwa miaka ya 2000, ilitungwa na Bunge lililoongozwa na
Spika Pius Msekwa, wakati Sumaye akiwa Waziri Mkuu na Kiongozi wa
shughuli za serikali bungeni.
Aliyasema
hayo wakati wa hafla ya kuzindua album ya waimbaji wa kwaya zilizo
chini ya Umoja wa Vijana wa Kipentekoste katika vyuo vikuu (UPSF)
vilivyopo mjini Morogoro jana, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Kwa
mujibu wa hotuba yake iliyopatikana kwa njia ya mtandao, Sumaye alisema
kumekuwapo matumizi mabaya ya takrima hasa wakati wa uchaguzi, akisema
inachochea rushwa. “Leo sote tu mashuhuda wa neno takrima kutumika kama
kichaka cha kujifichia wala rushwa,” alisema.
Aliongeza,
“sheria zote hutungwa kwa malengo mazuri, lakini katika matumizi yake
likijitokeza tatizo ambalo halikutegemewa, basi sheria hiyo hufanyiwa
marekebisho au kufutwa kabisa.”
Sumaye
alisema, “ni vizuri Bunge letu tukufu sasa likaifanyia sheria hiyo
marekebisho kwa kuliondoa kabisa neno takrima au kuipa tafsiri na
ufafanuzi ulio wazi zaidi, ili wala rushwa wasiitumie takrima kama
kichaka cha kujifichia.”
AKEMEA MAUAJI YA OPERESHENI
Sumaye,
amekemea mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola, dhidi ya raia wasiokuwa
na hatia ikiwamo kupitia operesheni zinazolenga kudhibiti uhalifu
nchini.
Sumaye
alisema, upungufu wa maadili mema ni tatizo kubwa katika jamii hivyo ipo
haja ya kuweka misingi imara ya kuondokana na tatizo hilo.
“Leo
kuna mauaji ya kutisha yanayotokea bila sababu zinazotosheleza, kama
vile watu kujitoa mhanga na kuua watu wengi wasio na hatia,” alisema.
Alitoa
mfano akisema, “hapa kwetu tumeshuhudia watu wakiteketeza familia nzima
kwa sababu tu kakosana na mpenzi wake, vyombo vya serikali kufanya
mauaji wakati wanafanya operesheni mbali mbali jambo ambalo wanajua ni
makosa.”
MISINGI YA HAKI
Sumaye
alisema wapo Watanzania wengi wanaoshindwa kupata haki zao mpaka `kutoa
chochote’, wakiwamo madereva barabarani wanaopata shida kupita bila
kuwahonga baadhi ya askari wa usalama barabarani.
“Na haya
yapo katika sehemu na sekta nyingi nchini. Ninapozungumza haya sijawahi
kusema hata siku moja kuwa rushwa hii imeanza sasa na huko nyuma
haikuwepo. La hasha! Rushwa imekuwepo hata kabla ya uhuru na imeendelea
kuwapo hadi leo,” alisema.
Aliongeza,
“hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikiri kuwa hata wakati
wa utawala wake rushwa ilikuwepo ila walikuwa hawana utani katika
kukabiliana nayo.”
Alisema
ipo haja kukubali kuwa rushwa ni tatizo linaloongezeka kwa kasi,
linaumiza uchumi wa nchi, wananchi na kuvunja heshima na hadhi ya taifa
kwa jumuiya za kimataifa.
AOMBA RADHI
Hata
hivyo, Sumaye aliomba radhi kwa kauli aliyonukuliwa Novemba 24, mwaka
huu mjini Moshi, akisema Tanzania inaongoza kwa rushwa katika Afrika
Mashariki.
“Hapo
niliteleza ulimi naomba radhi kama kuna waliokwazwa na hilo. Nilichotaka
kusema ni kuwa “rushwa ni tatizo linaloongoza Tanzania katika kuathiri
maisha ya watu wengi,” alisema.
AWAASA VIJANA
Aliwaasa
vijana kujiandalia maisha yatakayowawezesha kuchagia mabadiliko chanya
katika kuwapo utawala bora na kupiga vita maovu, kuimarisha uchumi.
Aliyataja mabadiliko mengine kuwa ni katika kupiga vita umasikini, kustawisha ulinzi na amani.
Sumaye
alisema, “kwa maoni yangu wasomi wetu hamjachukua nafasi yenu katika
nchi na labda hata katika jamii. Kuna mambo mengi makubwa yanayotokea
katika nchi lakini wasomi mnakaa kimya halafu yakisha haribika
tunatafuta wa kuwanyooshea vidole,” alisema.
Aliongeza,
“tuna maprofesa waliobobea wa fani mbali mbali, madaktari wahadhiri na
wanachuo wanaoweza kutufanyia uchambuzi na utafiti ili kuwa na mchango
chanya katika jambo lolote. Nafasi hii haijatumika ipasavyo na wakati
mwingine hata nahisi imetumika vibaya.”
Alisema
wanataaluma hao hawapaswi kuwaachia wanasiasa kila kitu pasipo kukosoa
na kuonya, badala yake kuwa mithili ya watazamaji na baadaye
walalamikaji.
AIPONGEZA UPSF
Alisema
UPSF ina umuhimu kwa jamii kwa sababu, pamoja na mambo mengine,
inawajenga vijana kiroho ili wawe watu wenye hofu ya Mungu.
Awali
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi wenye imani wa makanisa ya Pentekoste
Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Vicent Komba, alisema umoja huo
haufungamani na upande wala taasisi ya dini yoyote bali upo kwa ajili ya
kubadilisha watu kwa njia ya maombi na elimu kuweza kumrudia Mungu.
Alitaja
baadhi ya mambo ambayo umoja huo umekuwa ukipambana nayo kuwa ni
kuwabadilisha watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya, pombe, ukimwi na
masuala ya kifisadi ambayo yamekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini na
kusababisha madhara kwa kundi kubwa la vijana.
Alisema
kuwa hali hiyo pia imekuwa ikisababisha taifa kukosa viongozi bora na
wasio kuwa na maadili katika kuwatendea watu haki hivyo kupitia umoja
huo watahakikisha wanarudisha uhusiano chanya baina ya viongozi na
wananchi ili kuleta amani.
Walimhakikishia
Sumaye kuwa watakuwa naye bega kwa bega kwa kumfanyia maombi ili kila
kukicha wale wanaokusudia kumfanyia mabaya wasifanikiwe na yale
anayokusudia kuyafanya katika siku zake za usoni yafanikiwe baada ya
kuona mambo mazuri aliyofanya wakati wa uongozi wake alipokuwa
madarakani.
No comments:
Post a Comment