Pages

Sunday, January 26, 2014

China yachangia zaidi ya milioni 300 katika huduma za kijamii.

Lu YouqingBalozi wa China nchini Tanzania Lu Youqing
………………………………………………………………………………………
Na Immaculate Makilika –Maelezo.
Serikali ya Jamhuri ya watu wa China jana  katika uwanja wa Taifa wa  Uhuru jijini Dar es salaam imesheherekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano baina ya China na Tanzania ,ikiwa pia ni siku ya mwaka mpya wa kichina ambayo hujulikana kama sikukuu ya “Spring”.
Katika kusheherekea siku hiyo Serikali ya China pamoja na makampuni yamechangia zaidi ya milioni 300 katika huduma za kijamii,huku michango hiyo  ikiwa kama ifuatavyo; Serikali ya watu wa China imechangia milioni 100 kwa ajili ya kuchimba visima,Uhifadhi wa wanyamapori na mafunzo kwa wenyeji,wafanyabiashara wa China wamechangia milioni 50 kwa ajili ya visima na elimu huku Jumuiya ya Ujenzi wa Afrika wamechangia milioni 15 kwa ajili ya viatu vya wanafunzi.
Halikadhalika,Kampuni ya Madawa imechangia milioni 25 kwa ajili ya madawa ya kutibu malaria,huku milioni 100 zilichangwa na Jumuiya ya Muungano wa Wachina na fedha hizo zikielekezwa kwa vijana na wananchi wa Tanzania na kuhitimishwa na mchango kutoka Benki ya Biashara ya China ambayo imechanga milioni 20 kwa ajili ya vijana na elimu ya Tanzania.
Aidha ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji na Uwezeshaji Dr. Mary Nagu aliyekuwepo kwenye sherehe hizo kwa niaba ya Waziri Mkuu  Mizengo  Pinda, aliwashukuru sana watu Serikali ya China pamoja na wafanyabiashara na makampuni hayo  kwa misaada katika kuchangia maendeleo ya huduma za kijamii kwa watanzania.Urafiki wetu utaendelea kukua kwa faida ya watu wetu kama alivyosema waziri Nagu “China na Tanzania tunaurafiki wa dhati kwa muda mrefu sasa”.
Balozi wa China nchini Lu Youqing kwa upande wake alisema mwaka huu si tu kusheherekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lakini pia ni miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania.“Mwaka uliopita nchi hizi mbili zilikua na ziara kwa kiasi kikubwa ,huku tukishuhudia ujio wa Rais  wa China Xi jinping, hali hiyo imeleta msukumo mpya wa mahusiano unaolenga kuleta manufaa yenye usawa kwa nchi hizi mbili”.
Alisema watu wa China wamejidhatiti katika kujenga Taifa lao la China, watu wa Tanzania na Afrika kwa ujumla pia wamejidhatiti kufufua ndoto za maendeleo kwa nchi zao,tuungane sote pamoja katika kutimiza ndoto zetu za maendeleo katika mwaka huu mpya.
Sherehe hizo zilizohudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi wa China nchini,huku wakionekana wenye furaha wakati wote na kufuatilia kwa makini kila aina ya burudani iliyokuwa ikiendelea uwanjani hapo.
Bwana Jerome Wu,mwananchi wachina alisema hii ni mara yake ya tatu kuhudhuria sherehe za mwaka mpya wa kichina akiwa nchini Tanzania na kuongeza kuwa amefurahishwa sana na utofauti uliopo mwaka huu,na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali za nchi hizi mbili katika kudumisha urafiki huo na kuongeza kuwa yeye hupata fursa ya kukutana na jamaa na marafiki kwenye sherehe hizi.
Aidha viongozi mbalimbali wa Serikali na Jeshi  walihudhuria ikiwemo Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Asha Rose Migiro,Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Prof. Anna Tibaijuka na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Stephen Masele.
Uhusianao baina ya nchi hizi mbili ulianzishwa na Baba wa Taifa hayati Mwl Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong kwa nia ya kuhudumia wananchi wao,hatahivyo umekua ni uhusiano wenye manufaa makubwa kwa kusaidia kujengwa kwa reli ya Tanzania – Zambia,kiwanda cha nguo Urafiki, uwanja wa Taifa Uhuru, na miradi mingine ikiendelea ikiwa ni pamoja na  ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na bomba la gesi asilia toka Mtwara wakati miradi hiyo ikitazamiwa kuboresha uchumi na maisha ya watanzania pamoja na kudumisha urafiki huu baina ya Tanzania na China.

No comments:

Post a Comment