Pages

Thursday, January 23, 2014

IDADI YA WALIOPOTEZA MAISHA AJALI YA NOAH SINGIDA SASA YAFIKIA WATU 14...

Askari wakichukua moja ya miili ya waliofariki katika ajali hiyo eneo la tukio.
Mtoto wa miezi sita aliyejeruhiwa kwenye ajali ya gari dogo la abiria la Toyota Noah na lori la Scania mkoani hapa juzi, amefariki dunia na kufanya idadi ya waliokufa kufikia 14.
Happiness Elisha alifariki dunia jana akiwa katika Hospitali ya St Gaspar, Itigi alikokuwa amelazwa kwa matibabu. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa,  Geofrey Kamwela alisema jana, kwamba mtoto huyo na mama yake, Regina Masalu (27) baada ya ajali hiyo, walikimbizwa katika hospitali hiyo na wasamaria  waliofika eneo la tukio mapema.
Alisema Regina na mwanawe  ni wakazi wa Nkalankala wilayani Mkalama mkoani hapa na kwamba mama huyo anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo, na hali yake inaelezwa kuwa mbaya.
Aidha, Kamanda Kamwela alisema miili ya watu watatu ambao walikuwa hawajatambuliwa, tayari imetambuliwa kuwa ni ya Martin Marko (30) mkazi wa Itigi, Daniel Emmanuel (24) na Swalehe Hamisi (28) wote wakazi wa Saranda, Itigi.
Kamwela alisema abiria waliokuwa kwenye Noah, walikuwa 16 na si 14, kwa kuwa kuna majeruhi kwenye hospitali ya mkoa, ambaye anaendelea vizuri na mwingine yuko Hospitali ya Itigi.
Siku ya ajali, Noah ilikuwa ikitoka Itigi kuja mjini hapa, ndipo iligongana uso kwa uso na lori ambalo lilikuwa likitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam eneo la Isuna, barabara kuu ya Singida–Dodoma. Watu 13 waliokuwa kwenye Noah, walipoteza maisha papo hapo.

No comments:

Post a Comment