Pages

Friday, January 3, 2014

Kocha atua Yanga amfuta Kaseja


Kipa ya Yanga, Juma Kaseja.
Lucy Mgina na Khadija Mngwai
MABADILIKO yanaendelea kutokea ndani ya kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania, Yanga kwani tayari imepata kocha mpya wa makipa ambaye hata kabla ya kuanza kazi, ametangaza kumfuta kipa Juma Kaseja kama kipa namba moja.
Kaseja alipewa nafasi hiyo katika mechi yake ya kwanza akiwa amerudi Yanga na kufungwa mabao matatu wakati Yanga ilipolala kwa mabao 3-1 dhidi ya Simba katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Desemba 21, mwaka jana.
Juma Pondamali ambaye si mgeni kwa Kaseja ndiye kocha mpya wa makipa Yanga akichukua nafasi ya Mkenya Razack Siwa na amesisitiza: “Kwa sasa Yanga hakuna kipa namba moja.”


TUNAOMBA BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI ZA KILA SIKU,(USIPITWEEEEEEEE)

Kauli hii ya Pondamali maarufu kama Mensah inamaanisha Kaseja ambaye alilaumiwa kufungisha bao la tatu walipoivaa Simba, atalazimika kuwania namba dhidi ya Deougratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’.
Kipa huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, ameliambia gazeti hili kuwa kinachofuata kwake ni kazi tu na hatakuwa na utani hata chembe.
Kaseja alikuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Ernie Brandts na Siwa, halafu Deogratius Munishi ‘Dida’ akawa chaguo la pili huku Ally Mustapha ‘Barthez’ akiporomoka hadi chaguo la tatu ikiwa ni siku chache baada ya Kaseja kusajili Yanga.
“Kuanzia sasa hakuna kipa namba moja tena, nitawapa mazoezi ya uhakika mpaka wawe na viwango vya juu ninavyotaka. Makipa wote si wageni kwangu, nimewahi kuwafundisha katika timu ya taifa,” alisema Pondamali.
Akizungumzia juu ya ajira yake mpya klabuni hapo, Pondamali alisema: “Nimeshasaini mkataba wa miaka miwili Yanga na nimelipiwa kodi ya nyumba kwa mwaka mzima palepale nilipokuwa naishi Kigamboni (Dar es Salaam).
“Kuhusu usafiri, sijapewa gari binafsi ila nimekabidhiwa dereva ambaye atakuwa anatumia gari la klabu kwa ajili ya kuniendesha katika safari zangu za hapa na pale.
“Nashukuru Mungu mkataba wangu niliopewa hapa Yanga ni mzuri na kama ukizungumzia maslahi nadhani ni bora mara tano ya nilivyokuwa nalipwa Coastal Union na klabu nyingine zote nilizopita.”
Pondamali pamoja na Charles Boniface Mkwasa ambaye ni kocha msaidizi  mpya walitambulishwa jana katika kikao cha viongozi na wachezaji, ikiwa ni cha kwanza kukutana tangu kutangazwa kutimuliwa kwa Brandts na benchi la ufundi.
Mkwasa anakuwa kocha msaidizi huku Yanga ikiendeleza mchakato wa kumpata kocha mkuu na tayari zaidi ya makocha 40 wametuma maombi.
Aidha, Yanga imemrudisha daktari Juma Sufiani ambaye ilimuacha na nafasi yake kuchukuliwa na Nassor Matuzya ambaye pia ameachwa.CHANZO GPL

No comments:

Post a Comment