Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, January 27, 2014

Lipumba ahoji uzoefu wa Waziri wa Fedha

Profesa Ibrahim Lipumba
 
Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akitilia wasiwasi uzoefu wa kisiasa, kitaaluma na kiutawala wa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, waziri huyo amemjibu akisema anao uwezo na uzoefu mkubwa wa kuongoza wizara hiyo.
Profesa Lipumba jana aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema uzoefu wa Waziri Mkuya wa kuongoza Wizara ya Fedha unatia wasiwasi kutokana na unyeti wa wizara hiyo kulinganisha na wasifu (CV) wake uliobandikwa katika tovuti ya Bunge.

Alisema kwa mfano, CV hiyo inaonyesha kuwa alimaliza kidato cha sita mwaka 1995.
Profesa Lipumba alisema wakati huo (1995), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, alikuwa ni mmoja wa wataalamu bingwa duniani waliokuja nchini kuipatanisha serikali ya Tanzania na mashirika ya kimataifa kuhusiana na masuala ya fedha na uchumi, lakini sasa Waziri Mkuya amekuwa ndiye bosi wake.
Alisema pia CV ya Waziri Saada imetaja shule ya msingi alizosomea, lakini vyuo alivyosomea haikuvitaja.

Profesa Lipumba alisema CV hiyo pia inaeleza kuwa kati ya mwaka 2008 na 2010, Waziri Mkuya alisomea Shahada ya Uzamili ya Masuala ya Fedha, lakini chuo alichosomea hakikuelezwa na kusema kutotajwa chuo kunaweka wasiwasi wa ubora wa shahada aliyoipata.

Alisema baadhi ya wabunge aliozungumza nao, wamemueleza kuwa Waziri Mkuya amefanya kazi nzuri bungeni, hasa katika kipindi, ambacho aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk. William Mgimwa alikuwa mgonjwa.

Hata hivyo, akasema: “Ikiwa wasifu uliobandikwa katika tovuti ya Bunge ni sahihi ni wazi Mheshimiwa Mkuya hana uzoefu wa kisiasa, kitaaluma na kiutawala wa kuongoza wizara nzito na nyeti.

Akijibu, Waziri Mkuya alisema kuteuliwa kwake na Rais Jakaya Kikwete kumetokana na yeye kuonyesha uwezo wa kufanya kazi katika wizara hiyo. Alisema kabla ya uteuzi huo, ndiye aliyekuwa akikaimu nafasi ya waziri wakati Dk. Mgimwa anaumwa hadi alipofariki dunia. “Kuongoza siyo lazima uwe na elimu ya juu kama yake (Profesa Lipumba). Mheshimiwa Rais anamjua Benno Ndulu na mimi. Angetaka angemteua mtu mwingine yeyote,” alisema.

Alisema hajui kilichotokea kwenye tovuti ya Bunge, lakini CV imekamilika, ambayo inathibitisha vyuo mbalimbali alivyosomea katika nchi za Malaysia na Uingereza na katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (Out).

Waziri Mkuya alisema zaidi ya hivyo, ana uzoefu mkubwa wa kuongoza, ikiwamo kufanya kazi Wizara ya Fedha Zanzibar.

Alitaka Profesa Lipumba aulizwe ni wanafunzi wangapi aliowasomesha kwa sasa, ambao ni viongozi na pia alitoa maoni gani baada ya yeye (Waziri Mkuya) kuteuliwa kuongoza wizara hiyo?
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment