Pages

Sunday, January 26, 2014

Mahakama Nkasi yamuamuru mume kujenga nyumba ya mtalaka wake

Maria Tarafa (wa kwanza kushoto) akiwa na watoto wake wanne aliozaa na Ndebile Kazuri akiwa amekaa kwenye kifusi cha sehemu ya nyumba anayokaa, mumewe ameibomoa nyumba hiyo ili kumfukuza eneo hilo.MAHAKAMA ya mwanzo Mjini Namanyere, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imetoa amri ya kumtaka Ndebile Kazuri kujenga nyumba ya aliyekuwa mke wake Maria Tarafa iliyopo kijijini Isale ambayo aliibomoa akishinikiza mtalaka wake aondoke eneo ambalo alikuwa akikaa kabla ya kutengana.
Mwishoni mwa mwaka jana (2013) Mahakama hiyo ilivunja ndoa ya wanandoa hao wenye watoto wanne baada ya Kazuri kuwasilisha kesi mahakamani akitaka ndoa yake na mkewe ivunjwe. Hata hivyo baada ya kuvunjwa kwa ndoa hiyo mke amewasilisha kesi mahakamani hapo akitaka mali za ndoa hiyo zigawanywe na mume awajibike kuwatunza watoto wake, jambo ambalo halikuzungumziwa kwenye kesi ya awali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, Bi. Tarafa alisema Mahakama ya mwazo imetoa amri ya kumtaka mtalaka wake kujenga nyumba aliyomvunjia yeye na watoto wake wanne akishinikiza aondoke nyumbani hapo, bila kupewa haki ya mgao wa mali zilizochumwa wakati wa ndoa.
“…Juzi tumetoka Mahakamani nilikwenda kufungua kesi nikiiomba mahakama igawe mali ambazo tulichuma na mume wangu muda wote wa ndoa yetu lakini mume wangu hataki zigawanywe, ila mahakama imemuamuru kwanza ajenge nyumba ambayo amenivunjia pale nyumbani nikiwa na watoto akitaka niondoke nyumbani, ameambiwa awe ameimaliza kabla ya Februari 14,” alisema Bi. Tarafa akizungumza kwa njia ya simu.
Alisema Kazuri alivunja nyumba ambayo mkewe alikuwa akiishi na watoto wake wanne siku chache baada ya mahakama ya mwanzo wilayani Nkasi kuvunja ndoa yao, jambo ambalo Bi. Tarafa hakukubaliana nalo kwani alitegemea watagawana mali ya ndoa yao na yeye kupata nyumba ya kuishi.
“…Katika muda wote wa ndoa yetu tumefanikiwa kupata mali kama nyumba tatu ambazo zote zipo eneo moja la kijiji cha Isale, ng’ombe zaidi ya 127, mbuzi 30 pamoja na mashamba zaidi ya hekari 70 mali ambazo hazikuzungumziwa kabisa na mahakama, lakini baada ya ndoa kuvunjwa nashangaa mwenzangu ananibomolea hata nyumba ambayo nilikuwa naishi mimi na wanangu…sasa naomba kila mmoja agawiwe haki yake,” alisema Bi. Tarafa.
Kazuri alifungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya Nkasi Oktoba 28, 2013, kesi namba 26/2013 iliyosikilizwa na Hakimu aliyetajwa kwa jina la B. Stanley; na Novemba 18, 2013 hakimu huyo baada ya kuisikiliza kesi aliamuru ndoa ivunjwe.
Mahakama ilivunja ndoa hiyo na kuamuru Bi. Tarafa aondoke na watoto wawili kati ya wanne waliozaa na mumewe kipindi wakiishi kama mke na mume bila kueleza namna watoto hao watakavyo pata huduma toka kwa baba yao.
Mahakama pia iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao na wenye miaka chini ya saba kubaki na mama yao. Mahakama hiyo ya mwanzo pia iliamuru mke apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo walizalisha wote na bati 7 zilizokuwa nyumbani.
Kwa upande wake Kazuri akizungumzia juu ya mali ambazo mkewe anazilalamikia, alisema mali hizo alipewa na babayake wakati anaanza maisha hivyo bado ni mali ya babayake mzazi ambaye alidai yupo hai hadi sasa. Hata hivyo tarifa zaidi zinasema baba yake na Kazuri (Kazuri Moshi) alifariki mwezi Machi 2004 na mali zake kurithishwa kwa watoto wake akiwemo Kazuri.
Katika mgao huo mtalaka wa Kazuri alisema walipewa jumla ya ng’ombe 65 lakini wamezizalisha hadi kufikia idadi kubwa hivi sasa, ambapo ni zaidi ya ng’ombe 127 pamoja na mashamba.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA

No comments:

Post a Comment