Na Joachim Mushi, Nkasi-Rukwa
SAKATA la ndoa iliyovunjwa na mahakama ya Mwanzo
Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa limeingia katika sura mpya baada ya
uchunguzi zaidi kubainika kuwa mume aliyeiomba mahakama ivunje ndoa
yake, Ndebile Kazuri alimkatisha mke masomo ya elimu ya msingi mkewe
baada ya kumtia ujauzito akiwa darasa la sita.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ambazo mwandishi wa habari hii
amevipata vinaeleza kuwa Kazuri ambaye hivi karibuni ameiomba mahakama
hiyo kuvunja ndoa yake na Bi. Maria Tarafa kwa madai mke wake anakiburi
na mdokozi wa vitu ndani ya nyumba yao, alimkatisha masomo na baadaye
kumuoa mwaka 2004.
Taarifa zinaeleza kuwa Kazuri alimkatisha masomo Bi. Tarafa, mwezi
Machi akiwa Shule ya Msingi Isale iliyopo Wilayani Nkasi huku akiwa na
umri wa miaka 15 na alijifungua mtoto akiwa na umri wa miaka 16.
Taarifa zinasema baada ya kutiwa ujauzito Bi. Tarafa wazazi wa mumewe
walizungumza kifamilia na kukubaliana wasimshtaki kwa kuwa atafungwa na
mama na mtoto kukosa huduma za baba. Baada ya hapo walikubaliana amuoe
hivyo mume huyo alilipa mahari na kumuoa binti huyo wa darasa la sita
akiwa na umri wa miaka 16.
Akizungumza na Thehabari.com, kuzungumzia madai hayo Bi. Tarafa
amekiri kuwa ni kweli kwamba alikatishwa masomo na Kazuri mwaka 2003
akiwa darasa la saba, lakini kwa kuwa baba yake mzazi na baba mzazi wa
Kazuri walikuwa marafiki sana waliyamaliza wenyewe na kukubaliana watoto
wao waoane. Alisema aliunganishwa na mumewe Kazuri mwaka 2004 akiwa na
umri wa miaka 16 baada ya mumewe huyo kulipa mahari (ng’ombe) kwa
familia ya mzee Tarafa.
“…Inaniuma sana kwa kitendo ambacho ananifanyia kwa sasa kwani
alinikatisha masomo, kanipotezea muda wangu na kaniongezea mzigo wa
watoto wane na anataka niende kuishi nao peke yangu baada ya kwenda
kuongopa mahakamani,” alisema Bi. Tarafa.
Alisema sababu alizozitoa mahakamani si za kweli kwani amekuwa akimpiga na kumnyanyasa ndani ya ndoa yake na kumtaka aondoke kwake na kwenda kuishi kwao. Alisema kuna kipindi mtalaka wake huyo aliwahi kumfukuza akiwa na watoto wawili na kurudi nyumbani kwao lakini baadaye alikuja kuomba radhi na kutaka apewe mke wake aende kuishi naye.
Alisema sababu alizozitoa mahakamani si za kweli kwani amekuwa akimpiga na kumnyanyasa ndani ya ndoa yake na kumtaka aondoke kwake na kwenda kuishi kwao. Alisema kuna kipindi mtalaka wake huyo aliwahi kumfukuza akiwa na watoto wawili na kurudi nyumbani kwao lakini baadaye alikuja kuomba radhi na kutaka apewe mke wake aende kuishi naye.
Kazuri alifungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya
Nkasi Oktoba 28, 2013, kesi namba 26/2013 iliyosikilizwa na Hakimu
aliyetajwa kwa jina la B. Stanley; na Novemba 18, 2013 hakimu huyo baada
ya kuisikiliza kesi aliamuru ndoa ivunjwe. Mahakama ilivunja ndoa hiyo
na kuamuru Bi. Tarafa aondoke na watoto wawili kati ya wanne waliozaa na
mumewe kipindi wakiishi kama mke na mume bila kueleza namna watoto hao
watakavyo pata huduma toka kwa baba yao.
Katika hukumu yake mahakama iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki
kwa baba yao na wenye miaka chini ya saba kubaki na mama yao. Mahakama
hiyo ya mwanzo pia iliamuru mke apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10
ambayo walizalisha wote na bati 7 zilizokuwa nyumbani kwao.
Hata hivyo alipotafutwa Kazuri kuzungumzia madai hayo kwa njia ya
simu hakuweza kupatikana kwani taarifa ambazo zimetufikia ni kwamba, kwa
sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Nkasi kwa kitendo cha
kuvunja nyumba ya mtalaka wake na kumtishia kumdhuru huku akimtaka
aondoke kwake.
No comments:
Post a Comment