Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwakabidhi funguo ya boti na
"Life Jacket 8" kwa Uongozi wa kijiji cha Ilanga/Muze ikiwa ni sehemu
ya msaada wa boti na Injini moja kusaidia huduma za afya ya mama
wajawazito na wagonjwa mwambao wa Ziwa Rukwa. Msaada huo wenye thamani
ya Shilingi Milioni 20 umetolewa na Mfadhili Bi. Adrianne Strong kwa
kushirikiana na waumini wenzake wa Kanisa la University United Methodist
Church la Washington DC Marekani, Mfadhili huyo alishawishika kutafuta
msaada huo baada ya kufika Mkoani Rukwa katika kufanya utafiti na
kubaini mambo mengi ikiwemo umbali kati ya wananchi na vituo vya kutolea
huduma za afya.
Hapo awali yalifanyika majaribio ya Boti kabla ya makabidhiano rasmi.
Kabla ya makabidhiano ya Boti hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliamuru Boti hiyo kupelekwa ziwani kwa ajili ya majaribio.
Haikuwa
kazi rahisi kwani Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya
aliwaongoza viongozi wengine wa Chama na Serikali ya Mkoa na Halmashauri
kuvua viatu na kukanyaga maji ili kuweza kufikia Boti hiyo iliyobebwa
na wananchi wa kijiji cha Ilanga hadi ziwani.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiongea na wananchi wa Kijiji
cha Ilanga muda mfupi kabla ya kukabidhi msaada huo kwa uongozi wa
kijiji. Katika hotuba yake hiyo aliwashukuru wote waliosaidia
upatikanaji wa msaada huo ambao ni Bi. Adrianne Strong na waumini
wenzake wa Kanisa la University United Methodist Church la Washington DC
Marekani, Dkt. Francis Mashigala wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Rukwa
aliyekuwa anaratibu msaada huo na Bwana Hussein Kandoro (Mwanasheria
Ofisi ya Waziri Mkuu) aliyesaidia kusafirisha Boti hiyo kufika Mkoani
Rukwa. Kwa upande mwingine aliuita mwaka huu mpya 2014 kuwa ni mwaka wa
afya ambapo alihamasisha juu ya upimaji wa virusi ya Ukimwi, kupiga vita
unyanyapaa na Ukimwi, mama wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya
afya na kupeleka shule watoto wenye umri wa kwenda shule.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halamashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ndugu Adam Misana
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ilanga na kumkaribisha Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa kuzungumza na wananchi wake. Katika kauli yake alisistizia
agizo la Mkuu wa Mkoa wa Rukwa la kuhakikisha kuwa shughuli za uvuvi
katika ziwa Rukwa zinafungwa kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Januari
hadi Machi kupisha mazalio mapya ya Samaki. Alisema kuwa doria
zitaendeshwa katika Ziwa hilo na yeyote atakaekamatwa akivua katika
kipindi hicho hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Dkt.
Francis Mashigala wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Rukwa aliyekuwa mratibu
wa msaada huo wa Boti akitoa maelezo mafupi juu ya msaada huo kwa
wananchi wa kijiji cha Ilanga.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa na Msafara wake walipata fursa ya kutembelea Shamba
darasa la moja ya shule zilizopo katika kata ya Mtowisa kwenye kijiji
cha Ilanga ambalo limepandiwa kwa mbolea aina ya Minjingu Mazao.
Serikali ya Mkoa ikiongozwa na Injinia Manyanya ilitoa agizo kwa kila
shule kuwa na shamba angalao ekari tano zitakazotumika kama shamba
darasa na kusimamiwa na Afsa Ugani wa eneo husika na kupatiwa ruzuku ya
pembejeo inayotolewa Serikali.
Mpango
huo una faida mbili ambapo licha kuwa shamba darasa pia utatibu tatizo
la ukosefu wa chakula mashuleni na hivyo kuongeza mahudhurio na kuongeza
ufaulu kwa wanafunzi. (Na Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa @Rukwareview.blogspot.com)
No comments:
Post a Comment