KAMA Tembo wa Tanzania wangeulizwa kuna jambo gani kubwa hawatalisahau
kwa mwaka 2013, bila shaka jibu lingekuwa: “Tuliwindwa, tukauawa sisi na
watoto wetu na bado tuna hofu.”
Ingawa
tembo ni mnyama mbabe awapo porini, lakini uwezo wake wa kujilinda yeye
na jamii yake ulipunguzwa nguvu kwa kiwango kikubwa mwaka 2013, baada ya
mauaji ya hazina hiyo ya taifa kuongezeka kwa kiasi kikubwa hata
kuisukuma Serikali kuanzisha Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kila mwezi tembo 850 wanauwawa.
Utekelezaji
wa operesheni hiyo ambao ulilenga kuzuia uwindaji haramu wa wanyama hao
na wengine walio katika mbuga na hifadhi za taifa huku taarifa
zikionyesha kuwa shehena kubwa ya pembe za ndovu ambayo imekuwa
ikikamatwa ndani na nje ya nchi.
Ripoti ya
operesheni hiyo, ilileta athari kubwa kwa wananchi na mifugo hatua
iliyomlazimu Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne
waliokuwa wakiisimamia wizara zilizotajwa kuzembea katika kusimamia
Opereesheni Tokomeza Ujangili.
Mawaziri
hao ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis
Kagasheki, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Hata
hivyo, akizungumza katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais Kikwete
alisema: “Tunakamilisha matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya
Operesheni Tokomeza. Ni muhimu kuendelea nayo kwani tusipofanya hivyo
majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.
Kutokana
na kukithiri kwa matukio ya ujangili nchini, Mkataba wa Biashara ya
Kimataifa kwa Viumbe vilivyo Hatarini (CITES), uliitaja Tanzania kuwa ni
miongoni mwa nchi nane duniani zinazoongoza kwa kufanya biashara ya
pembe za ndovu.
Matukio yaliyotikisa
Polisi
mjini Zanzibar hawataisahau Novemba 15, 2013, siku waliyopigwa na butwaa
baada ya kukamata shehena kubwa ya pembe za ndovu katika Bandari ya
Malindi, zikiwa na thamani ya Sh7.4 bilioni.
Awali mzigo huo ulikuwa umehifadhiwa katika Mtaa wa Darajabovu, mkoa wa Mjini Magharibi, kabla ya kusafirishwa hadi Malindi.
Kamishna
wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema kuwa baada ya kukamilika kwa
kazi ya kupakua na kuhesabu pembe hizo, walibaini kuwa vilikuwa vipande
1,021 vikiwa na uzito wa kilo 2,915.
Tukio
jingine la kufunga mwaka ni lile lililotokea jijini Dar es Salaam,
ambalo lilisimamiwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis
Kagasheki na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Tarish Maimuna ambapo pembe za
ndovu 706 zilikamatwa.
Katika
tukio hilo, ambalo lilithibitisha kuuawa kwa tembo 353, raia watatu wa
China wakazi wa Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni, walikutwa
wakiwa wamehifadhi shehena hiyo nyumbani kwao.
Watuhumiwa hao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa Guandung. MWANANCHI
No comments:
Post a Comment