Mwanajeshi
wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), ambaye jina lake limehifadhiwa
anashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kuwaua kwa kuwapiga risasi
vijana wawili na kisha kuwajeruhi vibaya wengine wawili walipokuwa
katika shamrashamra za kuukaribisha mwaka mpya. Tukio
hilo lilitokea majira ya saa sita na robo usiku wa kuamkia jana, katika
eneo la Pugu Kinyamwezi, Ilala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na NIPASHE jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha
Minangi (pichani) alisema tukio hilo lilitokea baada kundi la vijana
waliokuwa wakisherehekea mwaka mpya kuzingira gari la mwanajeshi huyo
aliyekuwa akielekea nyumbani kwake Pugu Kinyamwezi, akitokea katikati ya
Jiji kwa shughuli zake.
Alisema mwanajeshi huyo alikuwa na gari aina ya Toyota Rava 4 na baada
ya kufika katika eneo hilo alizingirwa na kundi la vijana hao waliokuwa
wakisherehekea mwaka mpya na ndipo aliamua kutoa bastola yake na
kufyatua risasi ambapo iliwapata vijana hao na kufa papo hapo na
kujeruhi wengine.
Aliwataja waliokufa katika tukio hilo kuwa ni Ibrahim Mohamed(16) mkazi
wa Pugu Kinyamwezi, Abubakari Hassan(14) naye mkazi wa Pugu Kinyamwezi.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Rupano Wanga(17) mkazi wa Pugu Makange
na Kassim Abdul (16), mwanafunzi wa shule ya sekondari Tandika.
Minangi alisema polisi walifanikiwa kumkamata mwanajeshi huyo na kumweka
rumande katika kituo cha polisi cha Stakishari usiku huohuo.
Alisema vijana hao waliojeruhiwa walipelekwa Hospitali ya Amana kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Wakati huohuo, wakazi wa Kiwalani, Wilayani Temeke walipata wakati mgumu
baada ya kutokea kwa kundi la vibaka waliokuwa wakipora simu, fedha na
kutembeza mapanga kwa wakazi hao.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa maeeno hayo, kundi hilo lilikuwa
likizungukia kila nyumba na katika nyumba za starehe na kila aliyekutwa
nje walichukua simu yake, fedha na wengie kupigwa mapanga.
No comments:
Post a Comment