MKAZI wa
Kijiji cha Mwasutianga, Kata ya Irisya, wilayani Ikungi, Singida,
Mwanahamisi Mwangu (72), amekufa baada ya kupigwa mateke na ngumi na
mumewe, Salehe Mohammed (75) kutokana na ugomvi baina ya marehemu na mke
mwenzie wakigombea ndoo ya maji.
Tukio hilo limetokea Januari mosi mwaka huu, saa 7 mchana wakati wakiwa shambani wakipanda mazao.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alisema siku ya tukio
Mwanahamisi alikuwa shambani na mumewe pamoja na mkewe mdogo, Fatuma
Ramadhani (55). Walikuwa wakipanda mtama, lakini ghafla ulizuka ugomvi
wa kugombea ndoo iliyokuwa na maji.
Alisema katika ugomvi huo kila mmoja akidai ndoo hiyo ni mali yake, ndipo mume wao alipoamua kuingilia ugomvi huo.
“Mtuhumiwa mzee Salehe katika
ugomvi huo alikuwa upande wa mke mdogo ndipo alianza kumpiga mateke na
ngumi mkewe mkubwa Mwanahamisi na kusababisha kifo chake papo hapo,”
alisema Kamwela.
Alisema polisi wanamshikilia mtuhumiwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Katika tukio jingine, Shauri
Samwel (22) mkazi wa Kijiji cha Tyeme, wilayani Iramba, amefariki dunia
baada ya kunywa vidonge vya kuhifadhia nafaka.
Alisema
tukio hilo lilitokea Desemba 31 mwaka jana, saa 12 jioni katika
zahanati ya Kijiji cha Tyeme wakati Shauri akiendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda Kamwela alisema chanzo cha kunywa vidogo hivyo ni hofu aliyokuwa nayo Shauri kutokana na kumtia ujauzito binamu yake.
No comments:
Post a Comment