Pages

Tuesday, January 7, 2014

NI MARUFUKU DEREVA NA KONDAKTA WAKE KUMFUATA ASKARI WA USALAMA BARABARANI PINDI ANAPOSIMAMISHA GARI



 
KIKOSI cha Usalama Barabarani na Jeshi la Polisi mkoani Pwani, wamepiga marufuku kitendo cha madereva, makondakta wa mabasi, kushuka ndani ya magari yao na kwenda kupeleka kadi za gari kwa trafiki kibandani, nyuma ya gari ili ikaguliwe.
Agizo hilo limelenga kuzuia ushawishi wa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya makondakta na madereva wa mabasi dhidi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani. 
Akizungumza na Majira Mjini Kibaha, mkoani Pwani mwishoni mwa wiki, Kamanda Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, mkoani humo, Nassor Sisiwaya, alisema yapo malalamiko na hisia kwa baadhi ya watu kuwa, kondakta au dereva wa basi anaposhuka kupeleka kadi kwa trafiki ikaguliwe, huwa anatoa rushwa. 
"Kuna watu wanasema kadi anayoipelekwa kwa trafiki, huishikanisha na fedha ambayo humpa trafiki kama rushwa ili asimchukulie hatua za kisheria katika makosa ya usalama barabarani atakayokuwa ameyatenda. 
"Ili kuondoa mtazamo huo na vishawishi vya rushwa, nimepiga marufuku dereva au kondakta kushuka ndani ya gari ili kumfuata trafiki badala yake trafiki atapanda ndani ya gari, atakagua na kuuliza maswali hadharani mbele ya abiria," alisema.
Alisema askari wa Usalama Barabarani nchi nzima, wamekuwa wakilalamikiwa wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa hivyo yeye hayapingi malalamiko ya baadhi ya askari kuwa 
na tabia za aina hiyo ila si askari wote. 
Aliongeza kuwa, asilimia kubwa ya askari wa Usalama Barabarani ni waadilifu ambao wanatekeleza majukumu ya kazi zao na kusimamia sheria za barabarani kikamilifu.
Kamanda Sisiwayaalisema kama kuna trafiki mwenye ugonjwa wa kuomba na kupokea rushwa, aiombe na kuipokea hadharani mbele ya abiria. 
"Katika Stendi ya Mabasi Maili Moja, Kibaha, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama Barabarani ya Mkoa, tutafunga spika kubwa na kuwatangazia kondakta, madereva wasishuke katika magari yao wabaki ndani na kukaguliwa mbele ya abiria wao," alisema. 
Alisema jeshi hilo halitamvumilia askari ambaye itabainika anajihusisha na vitendo vya rushwa ambapo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake pamoja na kufukuzwa kazi. 
"Hatupo tayari kuona sifa za jeshi letu zikichafuliwa na askari wachache kwa tamaa ya pesa na kukiuka maadili ya kazi zao,viongozi tumejipanga kikamilifu kuwasaka, kuwakamata kwa ushirikiano na wananchi, tutamshughulikia ipasavyo ili iwe mfano kwa askari wengine," alisema. MAJIRA.

No comments:

Post a Comment