Pages

Wednesday, January 29, 2014

Operesheni Pamoja Daima: Itamtimua huyu bundi Chadema?




Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akihutubia moja ya mikutano katika Operesheni Pamoja Daima inayoendelea nchi nzima. Na Mpigapicha wetu
Mwaka 2013 ulimalizika vibaya kwa Chadema. Vivyo hivyo mwaka huu ulianza vibaya baada ya kuingiliwa na ‘bundi’ wa migogoro aliyepania kukipasua katika makundi mawili.
Hali hiyo iliendana na uamuzi mgumu wa Kamati Kuu ya chama hicho kuwavua nyadhifa za juu viongozi watatu – Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba. 
Kamati Kuu haikuishia hapo, baadaye ikawavua uanachama Dk Mkumbo na Mwigamba, huku Zitto akinusurika baada ya kufungua kesi mahakamani.
Athari za uamuzi huo zilisababisha baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya Chadema kutofautiana kimsimamo huku wengine wakifikia hatua ya kujiuzulu nafasi zao.
Miongoni mwa waliojiuzulu ni pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi na wenyeviti kadhaa wa mikoa, walioeleza wazi kuwa wanapinga Zitto kuvuliwa nyadhifa zake.
Mbaya zaidi ni pale mvutano huo uliposambaa hadi kwa mashabiki wa kawaida, nao wakaonekana kugawanyika katika makundi mawili, moja likimuunga mkono Zitto na jingine likibakia upande wa chama.
Hata hivyo, ingawa agenda hii haikuwekwa wazi, uongozi wa chama hicho umeibuka na mbinu ya kukabiliana na ‘bundi’ huyo wa mgawanyiko kwa kampeni maalumu iliyopewa jina la Operesheni Pamoja Daima, itakayofanyika katika mikoa tisa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anasema lengo kuu la kuanzisha operesheni hiyo ni pamoja na kukiimarisha chama na kuwafumbua macho Watanzania juu ya mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea. Operesheni hiyo ya siku 14 inayoendelea katika mikoa yote isipokuwa Lindi na Mtwara, inaendeshwa na makundi sita ya viongozi matatu yakitumia helkopta na wengine magari.
Swali la kujiuliza ni je, kufanyika kwa operesheni hii kutasaidia kumfukuza ‘bundi’ huyo aliyeanza kukipasua chama?
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema juhudi hizo zinaweza kufanikiwa kwa kiwango kizuri kwa kutegemea mwamko wa kisiasa wa mikoa wanayokwenda.
Ni njia sahihi
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiraia ya kufuatilia Utendaji wa Bunge (CPW), Marcossy Albanie anakubaliana na uamuzi wa chama hicho akisema operesheni hiyo ndiyo njia sahihi inayoweza kukiimarisha zaidi chama hicho. Albanie anasema harakati za kuanzisha operesheni hiyo ni pamoja na kuongeza mwamko wa Watanzania kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.  Anasema mgogoro uliojitokeza ndani ya chama hicho hauwezi kuwa sababu pekee ya kuanzisha operesheni hiyo.NA GAZETI LA MWANAINCHI

No comments:

Post a Comment