WAKATI
hatua zaidi zikisubiriwa kuchukuliwa kwa watendaji waliohusika na
ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa Operesheni Tokomeza, Rais Jakaya
Kikwete anatarajiwa kutangaza kuanza kwa awamu ya pili ya Operesheni
hiyo wakati wowote kuanzia sasa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu, alisema wakati wowote Rais Kikwete atatangaza kuanza
kwa Awamu ya Pili ya Operesheni Tokomeza na itazingatia haki zote
ikiwemo haki za binadamu.
Nyalandu
alisema ingawa awamu ya kwanza kulikuwa na kasoro zilizojitokeza, awamu
hii ya pili kasoro hizo zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha rasilimali za
Taifa zinalindwa.
Kusitishwa
kwa operesheni hiyo kulikosababisha uteuzi wa mawaziri watatu
kutenguliwa na waziri mmoja, kujiuzulu kwa mujibu wa Nyalandu,
kulisababisha pia tembo 60 kuuliwa.
Mawaziri
ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka jana
ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha
(Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo (Maendeleo ya
Mifugo) huku Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), akijiuzulu.
Katika
hatua nyingine, Nyalandu amemsimamisha kazi Ofisa Wanyamapori
Mwandamizi wa Pori la Akiba la Maswa, Lawrence Kileo, ambaye anatuhumiwa
kupokea rushwa na kuwatoza faini wafugaji wanaoingiza mifugo ndani ya
pori la akiba bila kuwapa risiti halali ya Serikali.
Pia,
ameamuru mamlaka husika kukamilisha uchunguzi na kuchukua hatua za
kinidhamu haraka dhidi ya Ofisa Wanyamapori wilayani Kasulu mkoani
Kigoma, Benjamin Mkasamali. Ofisa huyo anatuhumiwa kuwatorosha majangili
ambao waliwinda wanyamapori wasioruhusiwa kuwindwa katika kibali
kinachotolewa na Serikali.
Nyalandu
alisema Kileo amesimamishwa kazi, kutokana na makosa ya kupokea rushwa
na kuwatoza faini wafugaji wanaoingiza mifugo ndani ya pori la akiba
bila kuwapa stakabadhi ya Serikali, kinyume na Kifungu 116(2) (c) cha
Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya 2009.
Mkasamali
anachunguzwa baada ya Wizara kutumia njia za kiintelijensia na kubaini
kuwa aliingilia kati na kuwaachia huru majangili, waliokamatwa na kikosi
cha doria cha Kampuni ya Friedkin Conservation Fund.
Majangili
hao wanadaiwa kuwinda wanyama aina ya tohe 12, madume watano na majike
saba, ambao hawakuwepo katika orodha ya leseni yao ya uwindaji namba
B59921, iliyotolewa na ofisa huyo Novemba 29 /2013. Pia majangili hao
waliua wanyamapori wengine wanne aina ya oribi.
Alisema
baada ya Mkasamali kuwaruhusu majangili hao kuondoka, ambao tayari
walishakamatwa na kikosi cha doria, kiongozi wa kikosi hicho
aliwasiliana na RPC Kigoma, Freiza Kashai.
Inadaiwa
Kamanda Kashai alitoa ushirikiano kwa kumwagiza OC CID Kasulu, Athuman
Namba ambaye alishirikiana na Ofisa Usalama Taifa Kasulu, ambao kwa
pamoja waliweka kizuizi sehemu ya Kibagwe njia ya kwenda Kigoma na
kukamata majangili hao na kurudishwa Kasulu, ambako wamefunguliwa kesi.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment