Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ameiomba Jamhuri ya Watu wa China kusaidia mipangomiji katika baadhi ya
maeneo ya kimkakati ya Tanzania na China imekubali kuleta timu ya
wataalam kufanya tathmini katika maeneo hayo yote ama baadhi ya maeneo
hayo ili kujua mahitaji kamili ya mipangomiji ya maeneo hayo.
Rais Kikwete alitoa ombi hilo, Jumapili, Januari 12, 2014, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa
Nyumba, Makazi na Maendeleo ya Mjini na Vijiji wa China, Mheshimiwa Jiang Weixin, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Zanzibar.
Nyumba, Makazi na Maendeleo ya Mjini na Vijiji wa China, Mheshimiwa Jiang Weixin, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Zanzibar.
Rais
Kikwete alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu Tanzania Visiwani
ambako jana alishiriki katika Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya
Zanzibar wakati Mheshimiwa Weixin alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Watu
wa China Mheshimiwa Xi Jinping katika sherehe hizo.
Katika
mazungumzo hayo, Rais Kikwete alimweleza Mheshimiwa Weixin kuhusu
juhudi zinazofanywa na Serikali kuhusu umuhimu wa upangaji miji na
kuiweka miji ya Tanzania katika hali nzuri akisisitiza kuwa Serikali
inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa uwezo wa kiufundi, ukosefu wa
vifaa na ukosefu wa uwezo wa kifedha ili kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Rais
Kikwete amesema kuwa pamoja na kwamba changamoto za mipangomiji ziko
katika miji yote ya Tanzania, ikiwamo Dar es Salaam, lakini Serikali kwa
sasa inapenda kuelekeza nguvu zake katika miji mitatu ambayo ina uwezo
mkubwa wa kuendelea kwa kasi kubwa zaidi katika miaka michache ijayo na
hivyo lazima iendelee ikiwa imepangwa vizuri.
Rais
Kikwete ameitaja miji hiyo mitatu kuwa ni mji mpya wa Kigamboni, Dar es
Salaam na miji ya Mtwara na Lindi ambayo kwa sababu ya uvumbuzi wa gesi
na uchumi utakaotokana na uvumbuzi huo, inayo uwezo mkubwa wa kupanuka
na kukua kwa haraka na isipopagiliwa vizuri kutokea mwanzo inaweza
kuishia ikipanuka kwa ujenzi holela.
“Chukulia
mfano wa Jiji la Dar es Salaam Mheshimiwa Waziri. Mamilioni ya watu
wanaishi katika jiji hili lakini asilimia 70 ya mji huu haikupimwa na
imejengwa holela tu. Ni asilimia 30 ya Dar es Salaam iliyopimwa.
Hatuwezi kuiruhusu miji mingine, hasa ya kimkakati, kupanua na kukua kwa
namna hii.”
Baada
ya kumsikiliza Rais Kikwete, Waziri Weixin alisema kuwa ameelewa
changamoto zinazoikabili Tanzania na kuwa Wizara yake itatuma wataalam
wake kuja Tanzania kufanya tathmini katika maeneo muhimu kwa
kushirikiana na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi ambayo Waziri wake, Mheshimiwa Anna Tibaijuka alihudhuria
mazungumzo hayo.
Rais
Kikwete na Waziri Weixin pia walizungumzia hali ya uhusiano kati ya
nchi na wananchi wa nchi hizo mbili ambao utafikisha miaka 50, Mei,
mwaka huu, 2014, kufuatia kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya
nchi hizo mwaka 1964.
“Tanzania
imenufaika sana na uhusiano huu katika miaka 50 ilitopita. China
imeisaidia sana katika miaka 50 hiyo. Tunahitaji kuuendeleza uhusiano
huu na bado tunahitaji kuendelea kuungwa mkono na China kwa sababu
pamoja na yote, Tanzania bado ni nchi inayoendelea.”
No comments:
Post a Comment