JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KAZI NA AJIRA
TAMKO LA SERIKALI KUHUSU KUSITISHA UTARATIBU WA KUKODISHA WAFANYAKAZI UNAOFANYWA NA BAADHI YA WAKALA BINAFSI WA HUDUMA ZA AJIRA
1. Wizara
ya Kazi na Ajira imekua ikipokea malalamiko toka kwa wadau mbalimbali
kuhusu utaratibu wa udalali wa kukodisha wafanyakazi katika makampuni
unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini.
2. Wizara
imefanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hili na kubaini kuwa utaratibu
wa kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa
Huduma za Ajira ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya Mwaka
1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002]. Kwa mujibu wa
Kifungu 4 cha Sheria hii, majukumu ya msingi ya Wakala wa Huduma za
Ajira ni kuwaandaa na kuwaunganisha Watafuta Kazi na Waajiri kwa kutoa
mafunzo na ushauri elekezi kwa watafuta kazi, kutafuta fursa za ajira
na kutoa taarifa za soko la ajira. Hivyo, Mawakala hawapaswi kuwa
waajiri wa wafanyakazi waliowatafutia kazi kwa niaba ya Waajiri wengine.
3. Aidha,
uchunguzi umebaini kwamba utaratibu huu ni ujanja unaotumiwa na baadhi
ya Waajiri na Mawakala kwa lengo la kukwepa kodi na kujipatia faida kwa
kukwepa kutoa haki za msingi za wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria za
Kazi. Baadhi ya makampuni yanayokodisha wafanyakazi yamefanyiwa uhakiki
na TRA na kubainika kukwepa kodi ya mapato ya ajira (PAYE) na na kodi
ya mapato ya kampuni kinyume na Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kodi ya
Mapato ya Mwaka 2004 [Sura 332 kama ilivyorejewa Mwaka 2008].
4.Uchunguzi huu umebaini athari mbalimbali kwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu huu. Athari hizo ni pamoja na:
· Wafanyakazi
kukosa haki ya hifadhi ya jamii kama vile likizo ya uzazi na matibabu
kinyume na Sheria mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;
· Uwepo
wa ubaguzi katika malipo ya mishahara kwa kazi ya aina moja
kinyume na kifungu cha 7(10) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini
Na.6 ya mwaka 2004 ambacho kinamtaka mwajiri kuchukua hatua stahiki kwa
kuhakikisha kuwa wafanyakazi bila kujali jinsia zao wanalipwa mishahara
linganifu na ya haki kwa kazi yenye uzito na thamani sawa;
· Kukosa fursa za kujiendeleza kielimu na mafunzo;
· Kukosekana kwa usalama na uhakika wa ajira ;
· Wafanyakazi kulipwa mishahara ya kima cha chini kinyume na sekta wanayofanyia kazi.
5. Kwa
taarifa hii, Wizara ya Kazi na Ajira imeamua kusitisha mara moja
utaratibu wa Mawakalakuwaajiri wafanyakazi wanaowatafutia
kazi. Aidha, Mawakala na Kampuni husika waliopo katika utaratibu huu
kwa sasa wanapaswa kuwahamisha wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwa
Wakala kwenda kwa Kampuni husika. Waajiri na Wakala wanatakiwa
kukamilisha zoezi hili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na kuwasilisha
taarifa za utekelezaji kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira kabla au
ifikapo tarehe 28/02/2014.
6. Uchunguzi
zaidi unaendelea kubaini kama kuna wafanyakazi wa Kigeni wanaohusishwa
katika utaratibu wa kukodishwa ili hatua zinazotahili ziweze kuchukuliwa
ikiwa ni pamoja na kuwataka waombe vibali vya ajira kwa mujibu
wa Sheria ya Uhamiaji Na.7 ya mwaka 1995na Sheria ya Huduma za Ajira
Na.9 ya mwaka 1999. Wageni watakao kidhi vigezo wataajiriwa na kampuni
walipokodishwa; ambazo kwa wakati huo zitakua ndiyo mwajiri wao.
7. Wizara
ya Kazi na Ajira inawaelekeza Wakala wa Huduma za Ajira nchini kwamba,
kwa utaratibu wa sasa watapaswa kuwasilisha barua za maombi ya usajili
wa Uwakala kwaKAMISHNA WA KAZI kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya mwaka 1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002]
ili waweze kufanya shughuli za Uwakala wa Huduma za Ajira kisheria.
Maombi haya yawasilishwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu kutolewa
kwa tangazo hili. Baada ya muda huo Wakala asiye na kibali cha Kamishna
wa Kazi hatoruhusiwa kuendesha shuguli za huduma za ajira nchini.
Aidha, Mawakala watakaopata leseni ya Kamishna wa Kazi yatakua
yakitangazwa ili yatambuliwe na Umma.
8. Nasisitiza, maelekezo haya yatatolewa kwa Makampuni na Wakala waliohusishwa katika uchunguzi kwa ajili ya utekelezaji.
IMETOLEWA NA
GAUDENTIA MUGOSI KABAKA (MB)
WAZIRI WA KAZI NA AJIRA
27/01/2014
No comments:
Post a Comment