Ripoti
iliyotolewa na viongozi watatu wa zamani wa mashitaka ya uhalifu wa
kivita inasema kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kuwa
Syria imewatesa na kuwaua karibu wafungwa 10,000 tangu kuanza harakati
za kumpinga Rais Bashar Al-Asaad.
Wachunguzi
walipekua maelfu ya picha za wafungwa waliokufa zilizotolewa nchini
Syria na mpiga picha mmoja wa jeshi aliyetoroka kazi.
Wanasema miili mingi ilikuwa imekonda na mingine mingi kupigwa na kunyongwa.
Mmoja wa
waandaaji wa ripoti hiyo, Professa Geoffrey Nice, aliambia BBC kuwa
wingi na uhakika wa ushahidi uliotolewa unaonyesha wazi kuwa Serikali
ilihusika katika ukatili huo.
Uchunguzi
huo ulifadhiliwa na Serikali ya Qatar inayowaunga mkono waasi wa Syria.
BBC imejaribu mara kadhaa kupata majibu ya Serikali ya Syria kuhusu
madai hayo lakini Serikali haijatamka lolote.
Madai
kuwa wafungwa wamekuwa wakiteswa na kuuawa katika magereza ya Syria
yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na wakereketwa wa haki za kibinadamu
tangu maasi yaanze nchini humo miaka mitatu iliyopita.
Hata hivyo madai ya sasa yana upya fulani kwa njia ya kipekee.
Habari
hizi zina ushahidi kutoka kwa wandani wa Serikali wenyewe; mpiga picha
wa kitengo cha jeshi cha polisi aliyetoroka kazi amewasilisha maelfu ya
picha ambazo alipiga kabla ya kutoroka.
Na wachunguzi
wa kimataifa, waliokuwa viongozi wa mashtaka sasa wanaamini kuwa picha
walizoona za miili iliyoharibiwa vibaya, iliyopewa nambari na kupigwa
picha mara kadhaa, ni ushahidi wa kuaminika.
Zaidi ya
miili 11,000 ilipigwa picha ingawa bado kuna wasiwasi kuwa kuna maelfu
ya watu ambao walizuiliwa magerezani lakini sasa hawajulikani waliko.
No comments:
Post a Comment