Na Mwandishi wetu
WANANCHI
wa Mji mpya Relini wilaya ya Ilala waliopitiwa na mradi ya bomba la
gesi ya Mtwara wamemuomba Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Bi. Eugen Mwaiposa
awasilishe bungeni hoja ya kukataa mradi huo kutokana na kupunjwa fidia
ya nyumba na mali zao wanayotakiwa kulipwa.
Wakizungumza
na kutoa maazimio hayo katika mkutano wa dharura walioitisha na
kuhudhuriwa na mbunge wao, wananchi hao walisema awali walikubali mradi
huo kwa manufaa ya taifa lakini baada ya kuletewa dodoso la kutathmini
mali na nyumba zao wamegundua kuna ujanja unatumika kuwanyima haki na
kuwafanya kuwa masikini maisha yao yote.
Waliendelea
kudai kuwa mpaka sasa hawajui serikali imemkabidhi nani jukumu la
kuthamini nyumba zao kwani kampuni nyingi za ujanja ujanja zimejitokeza
kutaka kuwathamini lakini kwa kiwango cha chini ambacho hakiwezi
kumpatia makazi mengine.
Bw.
Josephat Haule alisema waathirika wenzao katika Kata za Kivule, Pugu
Kwalala na Mbande wao wamethaminiwa vizuri na wanatarajia kupata fedha
za kujenga nyumba nyingine kutokana na gharama kuwa juu lakini wao
nyumba iliyojengwa kwa sh. mil 57 anathaminiwa alipwe sh. mil. 11 na
nyumba zenye thamani ya sh. mil. 10 wanataka alipwe sh, mil 3.
Bw.
Robert Pius alisema kutoka taarifa ya Serikali itolewe ya kutangaza
kupitisha bomba la gesi eneo hilo waathirika wote walisimamisha
uendelezaji wa makazi hayo na kusubiri kupewa haki zao lakini ni mwaka
wa pili sasa hakuna taarifa zenye ukweli zinazowafikia hivyo kuwafanya
waishi kama wanya aina ya digidigi porini,
Mbunge
Mwaiposa akizungumza na wananchi hao aliahidi kushirikiana nao kujua
ukweli wa kampuni gani iliyopewa jukumu la kuthamini nyumba na mali zao
kwani anachofahamu ni kuwa Kampuni ya Kilwa Energy iliyopewa jukumu hilo
awali hakiwa na uwezo wa kifedha kuwalipa wananchi kwa wakati.
Aliahidi
kushirikiana na Kamati ya wananchi hao kushughulikia madai yao kwenda
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwenda kumuona Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, kwenda kumuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na
ikishindikana wanakwenda kumlalamikia Rais Jakaya Kikwete.
Alisema
wananchi wanateseka kwa vile kuhamisha makazi kutoka sehemu moja kwenda
nyingine kunarudisha maendeleo nyuma na kama anavyofahamu Serikali ya
Rais Kikwete ni sikivu na yenye kufanya kazi kwa ufasaha hajui sababu za
wananchi wake kushindwa kutimiziwa ahadi zao katika kiwango
kinachostahili.
"Wananchi
wangu wanadhiki, wanashida ya fedha lakini si kwa malipo kidogo kiasi
hicho, tunapiga picha tuoneshe umma thamani ya nyumba na kiasi
wanachotakiwa kulipwa ili wakaendelee na maisha yao sehemu nyingine"
alisema Bi. Mwaiposa.
Bi.
Mwaiposa alikiri kuona nyumba zilizothaminiwa kwa fedha kidogo ambazo
haziwezi kununua kiwanja kingine ambavyo kwa sasa katika maeneo hayo
vinauzwa kati ya sh. mil. 10 mpaka sh. mil. 15 kwa kiwanja cha nusu
hekari.
No comments:
Post a Comment