Lukata Singu
na baadhi ya wake, watoto na wajukuu zake katika picha ya pamoja. Picha
Elias MsuyaMzee Lukata Singu (65) anayeishi katika Kijiji cha Nyamwage
wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, anajivunia kuwa na familia kubwa yenye
wake wengi wanaofikia 15 na watoto zaidi ya 70.kijijini hapo ambapo
amejenga boma analoishi na baadhi ya wake, watoto na wajukuu.Singu
amenikaribisha nyumbani kwake na kutaka apate picha ya ukumbusho na
familia yake japo haijakamilika. Kisha anaanza kusimulia:"Mimi
nilizaliwa Shinyanga, sijui mwaka gani ila wakati Mwalimu Nyerere
anaanza kutawala wakati wa uhuru nilikuwa na miaka 13. Wazazi wangu
walihamia Tabora na baadaye Manyoni. Nimeishi Manyoni kwa muda mrefu
hadi nikawa na familia. Nimeishi pia Igunga na Tabora. Huko kote
nimeacha wake zangu na watoto," anasema Singu.Anasema alihamia wilayani
Rufiji miaka saba iliyopita akiwa na ng'ombe 600 hata hivyo wengi
walifia njiani wakati wa kuwasafirisha na magari.
TUNAOMBA BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI MOTOMOTO(USIPITWEEEE)
"Hapa
ninaishi na wake zangu 12. Wengine hawakuja hapa kupiga picha, wamebaki
kwenye maboma wanalinda vyakula. Hawa wengine unaowaona ni watoto na
wajukuu. Nina wake wengine watatu wilayani Igunga, Tabora na Manyoni,
kote huko nimeacha familia," anasema Singu.
Licha ya wingi wa wake na watoto, bado Singu anasisitiza kuwa hajaacha kuzaa kwani baadhi ya wake zake bado ni wajawazito.
"Siyo
kwamba nimemaliza kuzaa wala kuoa, tena baadhi ya wake zangu wana mimba.
Kwa nini niache kuzaa wakati bado nina nguvu?" anahoji.
Siri ya kuoa wake wengi
Singu
anaeleza siri ya kuoa wanawake wengi kuwa ni nguvu za kiume alizonazo
kulingana na umri wake mwenyewe akisema ni nguvu alizojaaliwa na
Mwenyezi Mungu.
"Ni uwezo
tu wa Mwenyezi Mungu, maana mimi nilizaliwa hivyohivyo, ndivyo Mungu
alivyoniumba... Situmii dawa yoyote. Kama Mungu asingeniwezesha
nisingekuwepo kwa sasa," anasema na kuongeza:
"Sina
dini yoyote, ila ninaamini Mungu yupo na ndiye anayeniwezesha. Huwa
ninamwomba na kumshukuru. Tumezaliwa tumemkuta kwa hiyo kusali ni
muhimu... naamini yupo na kama asingeniwezesha ningeshafutika."
Akizungumzia
elimu kwa watoto na wajukuu wake, anasema hiyo siyo kipaumbele kwake,
huku akisisitiza kuwa kuna uhaba wa shule katika kijiji hicho.
"Watoto
hawa hawasomi, tatizo huku hakuna shule, hata wenyeji wa huku hawasomi
kazi ni kukata miti tu. Hata hivyo kuna watoto wangu wako Tabora ndiyo
wamesoma, lakini sijui wamefikia darasa la ngapi," anasema.
Ndoa za utotoni
Mbali na
mzee Singu, yupo mjukuu wake, Jiraa Lukanda Lukata anayekadiriwa kuwa na
miaka 30 anayeonekana kufuata nyayo za babu yake.
Jiraa
ameoa wake watatu na anaishi na babu yake kwenye boma hilo. Kwa mke wa
kwanza, Gindu Shija mwenye umri wa miaka 21 ana watoto wanne huku mke wa
pili, Lawi Kulwa (miaka 21) na Holo Shija (miaka 15) walioolewa miaka
miwili iliyopita bado hawajapata watoto.
Hata hivyo, Jiraa anakanusha kufuata nyayo za babu yake:
"Siyo kwamba nafuata nyayo za babu, mimi naishia hawa wake watatu tu wanatosha," anasema Jiraa.
Akieleza taratibu za kupata wake hao, Jiraa anasema wazee hasa babu yake wamehusika kumtafutia.
"Kwa
taratibu zetu za Kisukuma, wazee huchunguza wanawake wenye tabia nzuri
kutoka kwenye koo nyingine. Hawa wake zangu babu yangu alinioza baada ya
kuridhishwa na tabia zao," anasema na kuongeza:
"Mke wa kwanza nilimwolea katika kijiji cha Muhoro hapa hapa Rufiji.
Akizungumzia
ufahamu wake kuhusu sheria za ndoa anasema licha ya kutokuwa na elimu
yoyote anazifahamu sheria zinazokataza ndoa za utotoni.
"Mimi
sina elimu yoyote wala wake zangu hawana elimu, lakini naelewa baadhi ya
sheria za ndoa. Najua sijafanya kosa kosa lolote kuoa wake wenye umri
huu," anasema.
Nao wake wadogo wa Jiraa Lawi na Holo wanasema kuwa wameridhika kuolewa naye.
Kuhusu elimu ya wake hao, Gindu, Lawi na Holo wanasema wamemaliza darasa la saba lakini hawajui kusoma wala kuandika.
Uhusiano na kijiji
Licha ya
kudai kuwa eneo analoishi katika kijiji hicho kuwa lake, inaelezwa kuwa
Singu hana uhusiano mzuri na wanakijiji wenzake.
Akiwa nyumbani kwake, Singu anasema maeneo yote yanayozunguka makazi yake anayamiliki kihalali.
Haya yote
unayoyaona hapa ni mashamba yangu, nimekuwa nikilima mihogo na mahindi.
Kwa sasa watoto wangu wanatayarisha mashamba kwa ajili ya kilimo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ibrahim Mboweto anasema kuna utata katika umiliki wa eneo hilo.
"Singu ni
kati ya wafugaji waliokuja na kuvamia maeneo ya vijiji. Baadaye
waliomba ndiyo akaruhusiwa. Lakini kwa kuwa ana mifugo mingi ilionekana
lile siyo eneo la mifugo na wananchi wanalalamika kuwa mifugo yake
inaharibu mashamba yake," anasema na kuongeza:
"Kuna
wakati alifukua kisima cha asili akawa akitumia kunywesha mifugo yake,
lakini aliwakataza wanakijiji wasikitumie, ndiyo nao wamekasirika
wanamlazimisha ahame. Mwenyewe amegoma akisema ili ahame wanakijiji
wamhamishe kwa gharama zao. Tumemwachia mkuu wa wilaya maana hatuna
uwezo tena."
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu amekiri kuufahamu mgogoro huo na kwamba anaushughulikia.
"Mgogoro
huo ulifika kwangu na nilifika kwenye mkutano wa kijiji, Singu
akaonyesha nyaraka zake za kumiliki hilo eneo," anasema Babu na
kuongeza:
"Yule
mzee alimilikishwa eneo na kijiji hivyo amewaambia kama wanataka ahame
inabidi wamlipe Sh90 milioni alizowekeza pale. Ndiyo nimewaambia
wanakijiji wasubiri wakati mwanasheria wangu anaangalia uwezekano
mwingine, wataambulia kesi."
Kuhusu
suala la elimu kwa wa watoto wake, Babu anasema amekuwa akihamasisha
jamii za wafugaji kupeleka watoto wao shule, ila kama hawataki ni juu
yao.
"Kila
ninapokuwa kwenye mikutano nawahamasisha hasa jamii za wafugaji wapeleke
watoto shule. Tumejenga shule nyingi na walimu wapo. Kuna baadhi ya
wafugaji wamewanunulia watoto wao baiskeli wanakwenda shule. Kama yeye
anaona starehe ni kuoa wake wengi na kuzaa, basi hiyo shauri yake,"
anasema Babu.
Utility
Kwa
mujibu wa sensa ya mwaka 2012, idadi ya Watanzania imefikia 44,928,923
ukilinganisha na idadi ya 12,313,469 ya mwaka 1967 wakati ambao kulikuwa
na ukuaji wa asilimia 2.9 kwa mwaka.
Watoto
walio chini ya umri kwa miaka 15 ni sawa na asilimia 44.1, huku walio
kati ya umri wa miaka 15 hadi 35 wakifikia asilimia 35.5, asilimia 52.2
ikiwakilisha kundi la watu wenye umri kati ya 15 hadi 64 na asilimia 3.8
ni kundi la watu wenye umri zaidi ya 64.
Idadi yay
a Watanzania inahusisha makabila zaidi ya 120 huku makabila ya
Wasukuma, Wahaya, Wanyakyusa, Wanyamwezi na Wachaga wakiwa na zaidi ya
watu milioni moja.
Mkakati
wa Kukuza uchumi na kupunguza umaskini (Mkukuta) umelenga kufikisha
huduma za kudhibiti uzazi kwa asilimia 60 ya wanawake wote ifikapo mwaka
2015 na utagharimu kiasi cha dola 88.2 milioni kati ya mwaka 2010 na
2015.
Hata
hivyo bajeti ya Taifa na utekelezaji wa mkakati huo umekuwa dhaifu licha
ya fedha za uzazi wa mpango zimeongezeka mara tatu tangu mwaka 2010
hadi 2011.
Licha ya
Serikali kuukubali mpango wa 'Kila mwanamke Kila mtoto' ambao ni wa
kwanza duniani na unaohamasishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban
Ki-moon kuhusu afya ya wanawake na watoto, Mpango wa maendeleo wa miaka
mitano uliotangazwa mwaka 2012 na Rais Jakaya Kikwete una kipengele
kimoja tu cha uzazi wa mpango.
No comments:
Post a Comment