Mtoto mchanga wa umri wa wiki mbili, ameuawa kwa kunyongwa
shingo na baba yake mzazi, katika ugomvi wa kifamilia, uliotokea katika
Kijiji cha Ibamba, wilayani Bukombe, katika Mkoa wa Geita.
Mtuhumiwa wa mauaji hayo ni kijana mfanyabiashara
wa umri wa miaka 28 ambaye inasemekana amekuwa katika mgogoro na mke
wake, Juliana Juma (20) tangu alipotoka mahabusu huko Biharamulo.
Habari zilisema mtuhumiwa huyo alikuwa anashikiliwa kwa tuhuma za kuiba mifugo.
“Alipotoka mahabusu mwaka jana, alikuta mke wake
akiwa na ujauzito na baada ya kujifungua, mwanaume alidai kwamba mtoto
si wake,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Kamanda wa polisi mkoani Geita, Leonard Paulo, alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku.
Alisema mtu huyo alimnyonga mtoto, wakati mkewe akiwa nje ya nyumba akifua nguo.
Kwa mujibu wa kamanda, baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa alitoweka nyumbani na kwenda kusikojulikana.
Kamanda Paulo alisema jitihada za polisi kumsaka na kumkamata mtuhumiwa hazijazaa matunda, lakini zinaendelea.
Mama mzazi wa mtoto huyo Juliana, alisema alikuwa na ugomvi na mume wake uliotokana na madai kwamba mtoto hakuwa wa kwake.
Alisema kauli hiyo ilikuja siku kadhaa baada ya yeye kujifungua mtoto huyo.
Kwa mujibu wa Juliana, mume wake alipotoka
mahabusu, alimkuta na mimba ya miezi mitatu na kuanza kumshawishi, ili
aitoe kwa madai kuwa haikuwa yake.
Alisema katika kipindi chote hicho, mume wake amekuwa akimtuhumu kwamba hakuwa mwaminifu katika ndoa yao.
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment