Pages

Saturday, February 15, 2014

BOMOABOMOA KABAMBE KUFANYIKA DAR.

Moja ya bomoabomoa zilizowahi kufanyika Dar.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ametangaza kuanza kwa bomoabomoa mpya kwa waliojenga katika maeneo ya wazi.
Alisema hayo jana wakati anafungua semina ya wahariri wa vyombo vya habari kuhusu sera na sheria ya ardhi na changamoto za wizara yake.
Huku akimshukuru Mungu kwa kuendelea kuwa kwenye wizara hiyo baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Profesa Tibaijuka alitamba kuwa waliokuwa wakisema yeye ni nguvu ya soda, wajue hajaisha na watamwona wiki ijayo.
“Nimepewa timu mpya na tumeshakubaliana kuwa tunaanza bomoabomoa. Watu walisema Profesa Tibaijuka ni nguvu ya soda, amekwisha…mimi sijaisha sasa nawatangazia wiki ijayo tunaanza bomoabomoa,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka, Dar es Salaam ndiko kwenye majambazi wa ardhi, ambao wamevamia maeneo ya wazi na kujitwalia na kujenga nyumba na maeneo sugu ni Sinza ambako wataanza kuona joto hilo wiki ijayo na kufuatiwa na Mbezi Beach. 
“Tulishawawekea taarifa ya kuhama, iliyobaki ni kuvunja. Tunajua wanakimbilia mahakamani, lakini tumejiandaa kitaalamu na tuna kikosi cha Polisi, tutavunja na tutakwenda mahakamani wanakokimbilia,” alisema.
Alifafanua kwamba utaratibu wa sasa wa uvunjaji maeneo hayo, watahakikisha wakati wakiendelea na kesi mahakamani, nyumba ya mvamizi wa eneo la wazi, itakuwa ‘imeshalala’ chini.
“Hapa kuna majambazi wa kupora ardhi, sasa nawapa taarifa wakati wao umekwisha…ukiwa na hati pandikizi, tutahakikisha nyumba imelala ndipo tunakuja mahakamani kutoa ushahidi,” alionya. Akizungumzia kukosa maadili kwa baadhi ya watendaji, Profesa Tibaijuka alisema katika wizara yake kulikuwa na ubovu wa mfumo uliokuwa ukisababisha  watendaji kuletewa vishawishi vingi.
Mbali na vishawishi, pia alisema mfumo huo uliwaweka katika mazingira ambayo mtendaji wizarani anaweza kuingizwa ‘mkenge’ baada ya watendaji wa halmashauri kushiriki rushwa na kutoa mapendekezo yanayokwenda kinyume na taaluma ya mipango miji.
“Sasa kuzuia hili, tumeondoa utaratibu wa hati kusainiwa na kamishna mmoja wa ardhi,  itasainiwa na watendaji kadhaa.
Tumeondoa utaratibu wa uhusiano wa bosi kumteremshia kazi mtu wa chini, sasa watu wanakaa pamoja wakiwa sawa kupitisha hati.
“Kabla ya kutoa hati, lazima ofisa mpimaji ajiridhishe kwanza ndipo watu wakae meza moja na kuitoa badala ya utaratibu wa zamani mtu mmoja kujifungia ndani na kusaini hati ya ardhi,” alisema Profesa Tibaijuka. 
Akizungumzia migogoro ya ardhi nchini, Profesa Tibaijuka alisema sekta ya ardhi ni ngumu na ugumu wake unaonekana pale mambo yanapokwenda kinyume na matarajio.
Alifafanua kuwa asilimia 80 ya malalamiko ya sekta hiyo yako nje ya uwezo wa wizara, kwa kuwa watendaji wa ardhi wako katika halmashauri, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Alisema matatizo mengi yako huko na uwezo wa Wizara ya Ardhi kusimamia changamoto za halmashauri kitaalamu ni mdogo.
Kuhusu mapigano ya wakulima na wafugaji, alifafanua kuwa hali ikifikia katika mapigano, huko ni kuvunja amani na chombo kinachohusika si Wizara hiyo, ila Wizara inaingia baada ya vyombo vya kutuliza na kurejesha amani kumaliza kazi.

No comments:

Post a Comment