Gharama kubwa za matibabu zawakatisha matumaini.
Hapa
duniani kuna maradhi aina nyingi yanayotisha, yakisumbua binadamu,
kuwatia ulemavu hata kuwa chanzo cha uchumi kutetereka, wakati mwingine
kusababisha kifo. Miongoni mwa maradhi hayo ni kuharibika kwa figo.
Ugonjwa
huo unaelezewa kwamba siyo tu unaleta maumivu kwa mgonjwa, bali pia
hautibiki kirahisi pamoja na gharama za matibabu husika kuwa kubwa na
wengi kushindwa kuzimudu.
Wataalamu
wa afya wanasema kuwa, zipo sababu kadhaa zinazosababisha maradhi
katika figo kwa binadamu ikiwamo matumizi mabaya ya dawa hasa za
maumivu, dawa za kienyeji, baadhi ya dawa za Kichina, uvutaji wa sigara
na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Onesmo
Kisanga, Daktari Bingwa wa Figo kutoka Hospitali ya Taifa
Muhimbili(MNH), Kitengo kinachoshughulika na tiba ya usafishaji wa figo
na damu(Renal Dialysis Unity) anasema kuwa tiba ya usafishaji wa figo
kwa kitaalamu (Dialysis), uhusika na utoaji wa maji yaliyojaa mwilini,
uchafu, pia sumu zitokanazo na vyakula au dawa. Dk Kisanga anasema kuwa
tiba ya 'Dialysis' ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji
kuipata, hutakiwa kutoa kiasi Sh300, 000, huku akitakiwa kuipata tiba
hiyo angalau mara tatu kwa wiki ambapo hugharimu Sh900,000.
"Hii
huduma inafanyika hapa (MNH) katika Kitengo cha Renal Dialysis Unity, na
mgonjwa anatakiwa kuipata tiba hiyo maisha yake yote,"anasema Dk
Kisanga.
Anafafanua
kuwa Dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitaji kutoka kwenye damu
ya mtu. Mchakato huo hufanyika baada ya figo kushindwa kufanya kazi na
taka hizo kuingia kwenye mfumo wa damu. Kwa kawaida figo hufanya kazi ya
kuchuja uchafu katika mwili, lakini baadhi ya watu huathirika na figo
zao kushindwa kufanya kazi ya kuchuja uchafu huo kutokana na sababu
mbalimbali zilizoainisha awali.
Kwa
mujibu wa Dk Kisanga, usafishaji wa figo hufanywa kwa wagonjwa ambao
figo zao zimeathirika kwa kiasi kikubwa na maradhi au hata kwa dharura.
Anafafanua
kuwa mgonjwa hutundikiwa mipira maalumu, huku kwenye mashine kukiwa na
figo ya bandia ambayo kazi yake ni kupitisha damu, kuisafisha na
kuirudishwa mwilini.
Anaelezea
kuwa kwenye mashine maalumu kunakuwa na mipira kadhaa ikiwamo ya
kupitishia damu kupeleka kwenye figo bandia, inayofanya kazi kama ya
mwilini na mirija mingine ambayo ni mikubwa kiasi inatumika kutoa maji
yasiyohitajika mwilini na sumu, huku mingine ikitumika kurudisha damu
safi mwilini.
"Mgonjwa
hulala akifanyiwa tiba hii kwa saa nne, bila kuchomwa sindano ya
usingizi, kwa kuwa haina maumivu makali. Vilevile mgonjwa hutobolewa
eneo maalumu mwilini kwa ajili ya kupitishia mipira. Kuna wanaotobolewa
shingoni au mkononi kulingana na anavyotaka mgonjwa," anasema Dk
Kisanga.
Anaongeza
kuwa pamoja na tiba hiyo kuwa ghali, bado haina uhakika wa kupunguza
tatizo kwa asilimia 100, bali kwa asilimia 40 hadi 50 pekee.
Mtaalamu huyo wa afya anaitaja tiba nyingine kuwa ni ya kupandikiza
figo, (kidney transplant) ambayo kwa sasa haifanyiki nchini. Hata hivyo
ili kufanyiwa upandikizaji huo nje ya nchi, mgonjwa anahitaji zaidi ya
Sh20 milioni.
"Tiba hii hufanywa hasa kwa mgonjwa ambaye figo yake imekufa na haiwezi kufanywa tena nchini," anasema Dk Kisanga.
Madhara ya tiba hizo
Hata
hivyo, Dk Kisanga anasema kuwa tiba ya figo ina madhara kiafya hasa kwa
walio kwenye hatua ya tano ya tiba hiyo. Madhara hayo ni pamoja na
maradhi ya moyo, miguu kukaza na maumivu ya kifua.
Kazi kuu za figo mwilini
Dk Kisanga anaeleza kuwa figo ni miongoni mwa viungo muhimu katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu.
Anasema
kuwa kwa kawaida, mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo
yanayofanana, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini
kidogo ya mbavu.
Anazitaja
kazi kuu za figo kuwa ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu katika
damu, kusaidia kuhifadhi,kudhibiti kiwango cha maji na madini
(electrolytes) mwilini.
Figo
huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo,
huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na
kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu
usiohitajika.
Anaendelea
kuwa kazi nyingine za figo ni pamoja na kusaidia kutengeneza kiasili
cha erythropoletin ambacho ni muhimu katika utengenezaji wa chembechembe
nyekundu za damu, hupokea asilimia 25 ya damu na kila figo ina
chembechembe hai ndogo milioni moja, pia kusaidia kudhibiti na
kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure).
Aina za ugonjwa wa figo
Dk Kisanga,
anazitaja aina za ugonjwa huu kuwa ni mbili; ya kwanza ni ile ya figo
kushindwa kufanya kazi kwa ghafla na muda mfupi; pili ni ile ya figo
kushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu.
Figo kushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu.
Daktari
huyo anasema kwa aina hii ya ugonjwa, figo huharibiwa taratibu na
kuendelea kupunguza uwezo wake wa kufanya kazi kadiri siku
zinavyokwenda.
Dalili za
aina hii ya ugonjwa huchelewa kujitokeza na wakati mwingine mwenye
tatizo hajisikii dalili yeyote, hadi pale inapotokea akaugua ugonjwa
mwingine na daktari kuhisi tatizo, ndipo hugundulika kuwa na ugonjwa huo
baada ya vipimo.
Sababu za figo kushindwa kufanya kazi ghafla
Dk Kisanga anaitaja sababu kubwa ni kupungua kwa mzunguko wa damu kwenye figo, kemikali za mwilini au kushambuliwa na sumu.
"Kushuka
kiwango cha mzunguko wa damu humpata mtu ambaye anatapika sana na hanywi
maji ya kutosha, anayeharisha sana na hanywi maji ya kutosha na wale
ambao hupoteza damu nyingi kama vile kwenye ajali," anasema Dk Kisanga.
Dk
Kisanga anazitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo,
moyo kushindwa kusukuma damu kwa ghafla, au waliougua maradhi ya moyo
kwa muda mrefu.
Kisanga
anazitaja kemikali kuwa ni pamoja na zinazotokana na kutumia dawa iliyo
na mzio kwa mtumiaji, dawa zinazosababisha mkojo utoke kwa wingi, dawa
za kienyeji na baadhi ya dawa za malaria.
"Tatizo
la figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla pia humpata mtu ambaye ana
bakteria kwenye mzunguko wa damu, ambao wanaweza kusababisha homa
'Septicemia' na kuugua malaria," anasema Dk Kisanga.
Anazitaja
sababu zinazofanya figo ishindwe kufanya kazi taratibu na kwa muda
mrefu na hatimaye kushindwa kabisa kuwa ni presha kuwa juu, kisukari,
magonjwa yanayosababishwa na bakteria, HIV, saratani na sumu mbalimbali
zinazoingia mwilini.
Dalili za figo kushindwa kufanya kazi vizuri
Dk
Kisanga anasema kuwa dalili ya kwanza ni kupungua kwa kiasi cha mkojo,
kushindwa kupumua, kusikia kichefuchefu, kutapika na kuvimba miguu.
Nyingine
ni maji kujaa mwilini, madini ya mwili kuwa juu hasa ya 'potashiamu',
asidi nyingi, matatizo katika moyo, ubongo, kukosa hamu ya kula na
kudhoofika mwili.
Anazitaja dalili nyingine kwa wagonjwa ambao hawagunduliki mapema ni kuvimba macho wakati wa asubuhi na uvimbe kupungua baadaye.
Nyingine
ni kuvimba miguu asubuhi, kupungukiwa damu mwilini kama dalili za kwanza
(kwani figo ikishindwa kufanya kazi ya kusaidia kutengeneza damu).
Ushauri
Dk
Kisanga anasema kuwa wakati tukielekea Siku ya Figo Duniani ambayo
hufanyika tarehe 13 Machi ya kila mwaka, ni vyema jamii ikaelewa kuwa
figo ni ogani inayohitahi utunzaji wa hali ya juu. Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment