Rais
Yoweri Museveni wa Uganda akisaini mswada wa sheria ya kupiga marufuku
ushoga, hapo jana jijini Entebbe, jambo lililoikasirisha Marekani. Picha
kwa hisani ya AFP.
Na Fadhy Mtanga
SERIKALI
ya Marekani imeanza mchakato wa kuupitia upya uhusiano wake na Uganda,
taifa la Afrika Mashariki baada ya rais wa nchi hiyo kutia saini mswada
unaoharamisha vitendo vyote vya kishoga nchini humo. Hapo jana, jijini
Entebbe, rais wa Uganda aliweka saini katika msaada huo ili kuwa sheria
rasmi ya Uganda. Kitendo hicho kimelalamikiwa sana na mataifa ya
Marekani na Uingereza kwa madai kinakiuka haki za kibinadamu.
Wizara
ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa taarifa kupitia kwa waziri wake, John
Kerry ikieleza kuwa serikali ya rais Barack Obama itahakikisha uhusiano
wake na Uganda unazingatia sera yake ya kuzuia unyanyasaji wa aina
yoyote.
Katika
taarifa hiyo iliyotumwa kwa barua-pepe kwenda kwenye gazeti la Daily
Nation la Kenya, Kerry amesema, "Kwa kuwa sasa hii sheria
imekwishapitishwa, tunaanza mchakato wa ndani kuhusiana na uhusiano wetu
na Serikali ya Uganda ili kuhakikisha namna zote za mahusiano yetu,
ikijumuisha misaada ya kimaendeleo zinaakisi dhima yetu ya kuondoa
unyanyasaji na ubaguzi."
Waziri
huyo wa mashauri ya kigeni wa Marekani amepigia chapuo kufutwa kwa
sheria hiyo. "Hii ni siku ya msiba mkubwa kwa Uganda na wote wanaojali
kuhusu haki za kibindamu. Kimsingi, suluhisho pekee ni kufutwa kwa
sheria hii."
Kuwekwa
sahihi kwa sheria hiyo kumewagutua Marekani, Uingereza na jumuiya
zingine zinazopigia debe mashoga kupewa haki. Tayari rais Barack Obama
ametoa taarifa kupitia kwa katibu wake kuwa, "rais wa Uganda amefanya
kitendo kichachostahili kujutiwa kwa kuwa ameirudisha nchi yake nyuma
badala ya kusimamia uhuru na haki sawa kwa watu wake."
Kerry,
katika taarifa yake ameeleza wazi kuwa Marekani imekuwa ikiupinga mswada
huo toka ulipofahamika miaka minne iliyopita. Ameeleza zaidi kuwa
sheria hiyo inakinzana na uwepo wa Tume ya Haki za Binadamu ambayo ipo
kwa mujibu wa katiba ya Uganda.
"Kutoka
Nigeria hadi Russia na Uganda, tunafanya kazi ulimwengu mzima
kuhamasisha na kulinda haki za kibidamu kwa watu wote. Marekani
itaendelea kusimama imara dhidi ya jitihada zozote kuwatenga,
kuwaharamisha na kuwaadhibu wahanga wowote wake katika jamii yoyote
ile." Alisema Kerry.
Kitendo
hicho cha Museveni kimeibua hisia kali kutoka kwa baadhi ya taasisi za
kimataifa ikiwemo makao makuu Umoja wa Mataifa jijini New York,
Marekani. Tayari Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameeleza azma yake ya
kulijadili jambo hilo la kupinga ushoga pindi atakapokutana na balozi wa
Uganda katika Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment