Askari polisi F. 5264 PC Sabato
(37) wa Kituo cha Polisi cha Longido, wilayani Monduli, ameuawa kwa
kupigwa jiwe na mtuhumiwa aliyekuwa akimpeleka mahabusu katika Gereza la
Kisongo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha,
Liberatus Sabas, alisema mauaji hayo yamefanywa na mtuhumiwa aliyekuwa
akipelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana katika kesi ya kuvunja na
kuiba.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, kesi hiyo iko katika Mahakama ya Wilaya ya Longido.
“Baada ya kufika njia panda ya Gereza la Kisongo, mtuhumiwa
alimwomba PC Sabato amfungue mkono ili ajisaidie haja ndogo, lakini
alipofunguliwa, ghafla aliokota jiwe na kumpiga askari huyo kwenye paji
la uso, akaanguka na kuzimia,” alisema Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas alisema kwa mujibu wa waendesha bodaboda
walioshuhudia tukio hilo, baada ya askari kuanguka chini, mtuhumiwa
alitumia pingu aliyokuwa amefungwa mkononi, kuendelea kumshambulia kabla
ya kutimua mbio.
Alisema hata hivyo waendesha bodaboda waliamua kumkimbiza na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.
Kamanda huyo alisema kitendo hicho kilifuatiwa na kutoa taarifa
katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege na baada ya muda,
askari walifika na kumchukua pamoja na majeruhi ambaye hata hivyo,
alifariki dunia usiku wa kuamkia jana, katika Hospitali ya Mkoa ya Mount
Meru.
Kwa mujibu wa Sabas, polisi wanaendelea kumhoji mtuhumiwa kabla ya kupandishwa kizimbani kwa shitaka la mauaji
No comments:
Post a Comment