Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI), Ramadhani
Madabida (kulia) na Ofisa Ubora wa Bidhaa wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD),
Evance Mwemezi walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam jana kusomewa mashtaka ya kuuza na kusambaza dawa feki za
ARV. Picha na Venance Nestory
Katika gazeti hili la Mwananchi linanza kwa kusema Mwenyekiti
wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Ltd cha Dar es Salaam (TPI),
Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la
kusambaza dawa bandia na kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.
Wakili
wa Serikali, Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa
na kesi hiyo kuwa ni Mkurugenzi wa Operesheni wa TPI, Seif Shamte,
Meneja Masoko, Simon Msofe, Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango pamoja na
wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD), Sadick Materu na Evans Mwemezi.
Akisoma
hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nyigulile
Mwaseba, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika shtaka la
kwanza, Aprili 5, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango wakiwa na
nyadhifa hizo kwenye kiwanda cha TPI walisambaza makopo 7,776 ya dawa
bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) aina ya Antirectroviral.
Kimaro
alidai kuwa washtakiwa hao, walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha
76 (1)(2) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003,
wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halali na kwamba
zimetengenezwa Machi, 2011 na muda wake wa kutumika unakwisha 2013
wakati wakijua kuwa si kweli.
Katika
shtaka la pili, Wakili Kimaro alidai kuwa Aprili 11, 2011, Madabida,
Shamte, Msofe na Shango walisambaza na kuuza makopo 4,476 ya dawa bandia
aina ya Antiretroviral walizokuwa wakijaribu kuonyesha kuwa zilikuwa na
viambatanisho vya Starudine 30mg, Nevirapine 200mg, Lamivudine 150mg
pamoja na fungu namba OC 01.85.
Alidai
kuwa washtakiwa hao waliweka viambatanisho hivyo wakijaribu kuonyesha
kuwa dawa hizo zilikuwa halisi na kwamba zilitengenezwa Machi 2011 na
muda wake wa kutumika ulikwisha Februari 2013 huku wakijua kwamba ni
uongo.
Katika
shtaka la tatu wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,
kinyume na Kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wakili
Kimaro alidai kuwa kati ya Aprili 12 na 29, 2011, washtakiwa hao wakiwa
na nia ya kulaghai, walijipatia Dola za Marekani 98,506 sawa na
Sh148,350,156.48 wakijaribu kuonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha ni
malipo halali ya makopo 12,252 ya dawa aina ya Antirectrovial yaliyokuwa
katika fungu (batch) namba OC 1.85.
Alidai
pia kuwa washtakiwa hao walikuwa wakionyesha dawa hizo bandia zilikuwa
zimetengenezwa Machi, 2011 na kwamba muda wake wa kumalizika kutumika ni
Februari, 2013 na wakafanikiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka
MSD.
Katika
shtaka la nne, Materu na Mwemezi wakiwa ni Meneja wa Udhibiti Viwango
na Ofisa Udhibiti Viwango wa MSD, kati ya Aprili 2 na 13, 2011 huku
wakijua nia ya kutendeka kwa makosa hayo ya usambazwaji wa dawa bandia,
walishindwa kuzuia kinyume na Kifungu cha Sheria namba 383 cha Kanuni ya
Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika
shtaka la tano, wakili huyo wa Serikali alidai kuwa kati ya Aprili 5 na
30, 2011, washtakiwa Madabida, Shamte, Msofe, Shango pamoja na Materu
na Mwemezi, kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi, walishindwa kutekeleza
majukumu yao wakiwa watendaji.
Alidai
kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa
kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kusambaza makopo 12,252 ya dawa
bandia wakijaribu kuonyesha kuwa zilitengenezwa Machi 2011 na kwamba
zitakwisha muda wake wa kutumika Februari 2013 na kuisababishia mamlaka
hiyo ya Serikali hasara ya Sh148,350,156.48.
Washtakiwa
wote walikana mashtaka yanayowakabili na upande wa mashtaka ulisema
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Akitoa masharti ya dhamana,
Hakimu Mwaseba alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili
wanaoaminika ambao wanafanya kazi kwenye taasisi zinazotambulika
kisheria na kwamba kila mdhamini angesaini bondi ya Sh6,181, 256.
Pia
alimtaka kila mshtakiwa kutoa kiasi cha Sh12, 362,513 milioni taslimu
mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi
hicho cha fedha.
Madabida na Materu waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo huku wenzao wakipelekwa mahabusu kusubiri kuyakamilisha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, mwaka huu itakapotajwa.
No comments:
Post a Comment