Moja
ya picha mbalimbli za Tembo zilipamba ukumbi yalipofanyika majadiliano
kuhusu tembo, picha hizo na ambazo zilikuwa kivutio kwa washiriki wa
majadiliano hayo ziliandaliwa na National Geograpy.
Mkurugenzi
Mtendaji wa ABC HOME Paulette Cole akiwakaribisha wanajopo na wageni
waalikwa katika majadiliano kuhusu tembo, majadiliano hayo yalifanyika
siku ya jumanne usiku Jijini New York.
Chelsea
Clinton, Makamu Mwenyekiti wa Clinton Foundation, na ambaye aliongoza
majadiliano hayo akiwatambulisha wanajopo, kutoka kushoto ni Bw. John
Heminway, Balozi Tuvako Manongi, kati kati ni Chelsea Bint wa Rais Bill
na Hilary Clinton, kulia kwa Chelsea ni Bw. Bryan Christy na anayefuatia
ni Bw. Josh Ginsberg kutoka Wildlife Conservation Society. Heminway na
Christy ni waandishi na watunga filamu na kwa pamoja wametengeneza
filamu ijulikanayo kama "The Battle for Elephants". Filamu hiyo
itaonyeshwa February 27 kupitia Channel ya National Geograpy.
Muwakilishi
wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Manongi,
akielezea jambo wakati wa majadiliano kuhusu tembo na changamoto
zinazomkabili. Balozi Manongi alitumia fursa hiyo kuelezea juhudi
mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya
ujangili na udhibiti wa biashara haramu ya pembe za tembo.
Bw.
Bryan Christy naye akieleza jambo, Bw. Christy ameshiriki katika
kutengeneza filamu ya The Battle for Elephants, habari zaidi zinaonyesha
kwamba sehemu ya filamu hiyo inahusu Tanzania, na Bw. Christy
anaonekana kwenye filamu hiyo akipozi kama mnunuzi wa meno ya tembo.
Sehemu ya washiriki waliohudhuria majadiliano hayo ambapo pia walipata fursa ya kuuliza maswali kwa wanajopo.
Hapana
shaka kwamba Hatari ya kutoweka kwa tembo barani afrika, ni jambo
linalowagusa wengi, washiriki wa majadiliano hayo walitumia fursa hiyo
kujifunza siyo tu hatari ya kutoweka kwa mnyama huyo, lakini pia uzuri
na sifa zake, na namna gani wanaweza kuchangia kuhakikisha hatoweki
kabisa.
Waandishi
pia walikuwepo nao walipewa changamoto ya kuandika habari zenye
kuelimisha jamii kuhusu athari za mauaji holela ya tembo pamoja na
kuihamasisha kutambua wajibu na nafasi yao katika uhifadhi wa wanyama
walio katika hatari ya kutoweka.
Pichani ni sehemu ya washiriki wa majadiliano hayo
Na Mwandishi Maalum
Zikiwa zimepita wiki chache tangu kufanyika kwa Mkutano uliojadili
kwa kina kuhusu ujangili dhidi ya tembo na biashara haramu ya pembe za
tembo uliofanyika Jijini London, Uingereza. Jana Jumanne, hapa Jijini
New York, Marekani, palifanyika majadiliano mengine yakihusu pia sifa na
uzuri wa mnyama tembo na hatari inayomkabili.
Majadiliano hayo na ambayo yaliwavutia washiriki wengi,
yaliandaliwa kwa ushirikiano kati ya National Geograpy na ABC na
yalifanyika katika jengo lijulikanalo kama ABC HOME lilipo Broadway,
jijini New York.
Balozi Tuvako Manongi, Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alikuwa kati ya wanajopo wanne
walioalikwa kushiriki majadaliano hayo ambayo yaliongozwa na Chelsea
Clinton, Makamu Mwenyekiti wa Clinton Foudantion.
Wanajopo wengine walikuwa ni Bw. Josh Ginsberg kutoka Wildlife
Conservation Society, Bw. John Heminway mwandishi na mtengeneza filamu
ambaye pamoja na mwanajopo mwingine Bryan Christy wameshiriki katika
kutengeneza filamu ijulikanayo kama “The Battle for Elephants” filamu
hii inatarajiwa kuonyeshwa february 27 kupitia Channel ya National
Geograpy.
Wanajopo hao wakiongozwa na Chelsea Clinton, walipata fursa ya kila
mmoja wao kuelezea nini yeyé kama mtu binafsi au kupitia taasisi
anayoiwakilisha ametoa mchango gani katika suala zima la uhifadhi wa
Tembo na uthibiti wa mauaji holela ya Tembo na biashara haramu ya pembe
za tembo.
Balozi Manongi kwa upande wake, alielezea juhudi mbalimbali ambazo
serikali inafanya katika kukabiliana na ujangili dhidi ya tembo, pamoja
na biashara haramu ya pembe , aidha alielezea dhamira na nia ya serikali
ya kuendeleza mapambano ya kuwanusuru tembo kupitia awamu ya pili ya
Operesheni Tokomeza.
Balozi pia alijibu maswali mbalimbali na kutolea ufafanuzi hoja
zikiwamo kuhusu kwanini operesheni tokomeza ilisitishwa, na je serikali
ilikuwa na mpango gani kuhusu shehena ya pembe za ndovu ambayo iko
katika maghala.
Kwa ujumla wanajopo wote walikubaliana kwamba, mapambano dhidi ya
ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu ni vita ngumu hasa
ikizingatiwa kwamba mtandao unaohusika na biashara ya pembe za tembo ni
mpana sana na unaohusisha watu wengi.
Na kwa sababu hiyo wamehimiza mambo kadhaa yakiwamo, ushiriki wa
wadau kutoka makundi mbalimbali ya kijamii kitaifa na kimataifa,
udhibiti wa soko na hitajio la pembe za ndovu, utoaji wa elimu kwa umma,
uwezeshwaji wa watendaji katika ngazi mbalimbali, na uimarishaji wa
sheria.
No comments:
Post a Comment