Mechi kati ya Azam FC na Ferroviariao ya hapa Beira Msumbiji imepangwa kupigwa kuanzia saa 9 alasiri za hapa Msumbiji sawa na saa 10 za nyumbani Afrika Mashariki.
Jambo lingine muhimu la kufahamu ni kuwa timu imefika hapa Jumatano usiku ni Jumamosi tu jua lilitoka na mvua haikunyesha kabisa.
Lakini leo tangu alfajiri mvua kubwa imekuwa ikinyesha na anga limetanda mawingu mazito; dalili kuwa mvua itaendelea kunyesha kwa muda mrefu kutwa ya leo.
Kwa muda wote Azam imekuwa ikifanya mazoezi katika viwanja vilivyojaa maji. Mara ya mwisho kufanya mazoezi katika uwanja utakaotumika kwa mchezo leo ilikuwa Ijumaa alasiri na sehemu kubwa ya uwanja ilikuwa imejaa maji.
Kwa mujibu wa Kanuni za CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika) zinazoendesha mashindano ya Kombe la Shirikisho, mchezo wowote ambao haukumalizika kutokana na hali mbaya ya uwanja (pitch) au hali mbaya ya hewa, utachezwa ndani ya saa 24 baadaye.
Kanuni ya 7(7)inasomeka "Ikiwa mchezo utasitishwa kabla ya muda wa mchezo kumalizika kwa sababu zilizo nje ya uwezo hususan kwa sababu ya hali mbaya ya uwanja na/au hali mbaya ya hewa kwa uamuzi wa mwamuzi, mchezo huo utachezwa saa 24 baadaye katika uwanja uleule na waamuzi walewale. Hatua zote za kinidhamu (kadi za njano na nyekundu) zilizochukuliwa wakati wa mchezo uliovunjika zitabakia kwa mujibu wa Kanuni ya adhabu ya CAF".
Suala la mvua na hali ya uwanja lilijitokeza na kujadiliwa wakati wa kikao cha matayarisho ya mchezo kilichofanyika jana katika Hoteli ya Tivoli hapa Beira.
Kamishna wa mchezo wa leo Charles Kafatia kutoka Malawi aliwaambia wawakilishi wa klabu mbili na waamuzi kutoka Zambia wakiongozwa na Wisdom Chewe kuwa iwapo uwanja utaendelea kuwa katika hali isiyoridhisha basi kanuni zitafuatwa na mwasiliano kupelekwa CAF.
Kwa mujibu wa ratiba ya kiutawala, Kamishna Kafatia akifutana na mwamuzi wa akiba atakwenda uwanjani saa 4 asubuhi hii kukagua masuala muhimu ikiwepo sehemu ya kuchezea na taratibu za kiusalama.
OMOG asema, Kuvuka raundi ndiyo malengo ya timu yake
Kocha Mkuu wa Azam Joseph Omog amesema timu yake itaingia dimbani kuwakabili wenyeji Jumapili Ferroviario da Beira kwa lengo moja tu la kufuzu kwa raundi inayofuatia katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Omog amesema matayarisho yote yamekwenda sawa katika muda wa siku tatu ambazo wamekuwa hapa Beira na kubainisha kuwa wachezaji wake wote wako katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo huo muhimu wa marejeano.
“Tumefanya mazoezi kwa siku tatu, hatuna matatizo makubwa ya kutukwaza, jambo pekee ambalo si sawa ni hali ya mvua ambayo imesababisha viwanja kujaa maji, alibainisha Omog.
Huku akitambua changamoto inayoikabili timu yake katika mchezo huu wa marejeano baada ya kupata ushindi wa 1-0 la Kipre Tchetche Jumapili iliyopita jijini Dar es Salaam, kocha Omog amesema wanachukua tahadhali zote kimchezo kwa kuwaelekeza wachezaji wake wanacheza kwa lengo la kupata magoli na iwapo magoli yatashindikana basi wazuie kwa umoja na kuepuka kuruhusu goli langoni mwao.
“Mpango ni kuhakikisha tunamiliki mpira kuliko wapinzani wetu, tunaponyang’anywa mpira lazima tujitahidi kuurejkesha mpira kwenye miliki yetu mapema iwezekanavyo na hii ni kazi ya timu nzima ambayo itatuwezesha kutimiza malengo yetu” alinena mkufunzi huyo bingwa wa kombe la Shirikisho mwaka jana akiwa na klabu ya AC Leopards ya Kongo Brazaville.
Kuhusu utelezi uwanjani amabao unaweza kuvuruga mipango ya timu yake Omogo alisema maelekezo kwa wachezaji wake hususan wa safu ya ulinzi ni kuhakiksha hawaruhusu mipira kuzagaa katika eneo lao, hivyo lazima waihamisha haraka kuepusha hatari.
Aliongeza kuwa baada ya kuwaona wapinzani wao katika mchezo wa kwanza, amebaini kuwa wanapendelea kutumia mipira mirefu, hivyo amesema hilo ni eneo lingine muhimu ambalo amelitilia mkazo wakati wa mazoezi.
Mwantika Arejea kikosini
David Mwantika ambaye hakucheza mchezo wa kwanza kwa kuwa alikuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonesha kwenye wa mwaka jna dhidi ya FAR Rabat ya Morocco anarejea leo na mwalimu Omog ameamua kumpanga sehemu ya beki wa kulia ili kuimarisha eneo la ulinzi.
Kikosi kitakachoanza leo ni Mwadini Ally, Erasto Nyoni, David Mwantika, Aggrey Morris Said Morad, Michael Bolou, Himid Mao, Salum Abubakar Brian Umony, Kipre Tchethche na Mcha Hamis.
Mwalimu Omog anazo bunduki zake nyingine benchi kama nahodha John Bocco ambaye amerejea kutoka majeruhi na Dar es Salaam aliingia kipindi cha pili. Pia wapo Jabir Aziz aliyecheza pia kipindi cha pili, Malika Ndeule, Ismael Kone, Aishi Salum na Ibrahi Mwaipopo
Watanzania watoa sapoti kubwa
Jumuiya ya Watanzania waishio hapa Msumbiji wakiongozwa na Richard Alloyce wamejipanga vilivyo kuishangilia Azam na wamekuwa wamsaada mkubwa kuelekea mchezo huo.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano, dakika 90 zikimalizika bila mshindi kuamuliwa, itatumika changamoto ya mikwaju ya penati. Omog amesema timu yake imejiandaa kwa mazingira yote.
Iwapo Azam itafaulu kuitoa Ferroviario itakabiliana na Zesco ya Zambia,ikianzia nyumbani kati ya Machi 1 na 2 mwaka huu
No comments:
Post a Comment