Mtuhumiwa
wa mauaji ya watu tisa na unyang'anyi wilayani Tarime mkoani Mara,
aliyekuwa akihojiwa Polisi kwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili,
amefariki katika Hospitali ya Wilaya wakati akipatiwa matibabu ya
ugonjwa wa pumu.
Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya, Kamishina Msaidizi Justus
Kamugisha, alisema kuwa mtuhumiwa huyo jina lake halisi ni Charles
Kichune (38) na alifariki usiku wa kuamkia jana wakati akitibiwa ugonjwa
huo hospitalini.
Majina mengine aliyokuwa akiyatumia kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha ni pamoja na Josephat Chacha na Charles Msongo.
"Mwili wa marehemu upo chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya
ukisubiri kufanyiwa uchunguzi na kuchukuliwa na ndugu zake," alisema
Kamanda Kamugisha.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda Kamugisha, Kichune baada ya
kukamatwa alikiri Polisi kuhusika katika mauaji ya watu mbalimbali
katika kata za Binagi, Turwa na Kitare katika vijiji vya Mogabiri,
Kenyamanyori, Nkende na Rebu.
Kamanda Kamugisha alisema mtuhumiwa huyo Kichune alikamatwa Februari
6 mwaka huu mkoani Tanga baada ya Polisi kufuatilia mtandao wake baada
ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Baada ya kukamatwa, uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa baada ya
mauaji ya watu tisa, mtuhumiwa alikodisha pikipiki kutoka kijiji cha
Kenyamanyori alikokuwa akiishi, hadi Musoma.
Alipofika Musoma, inadaiwa alihifadhi bunduki aina ya SMG na risasi kadhaa kwa mshirika wake, Marwa
Keryoba maeneo ya Bweri na alipokamatwa alimtaja Keryoba kuwa ndiye anayetunza silaha hiyo.
Februari 7 mwaka huu, Polisi walifuatilia silaha hiyo kwa Marwa na
kumkuta mtuhumiwa, ambapo alitakiwa kujisalimisha lakini alikaidi na
kuanza kurushia risasi askari.
"Marwa aliuawa Februari 7 alfajiri Bweri Musoma, wakati alipotakiwa
kujisalimisha na kukaidi na kuanza kurushiana risasi na askari," alisema
Kamanda Kamugisha.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, kuna mtuhumiwa mwingine sugu wa
mauaji ya watu zaidi ya 10, Senso Magabe ameuawa katika majibishano na
Polisi wiki iliyopita.
Hata hivyo katika majibishano hayo, wenzake watatu walifanikiwa
kutoroka na msako unaendelea wilayani hapa ambapo wananchi wameombwa
kutoa ushirikiano Polisi ili kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Kamanda Kamugisha alisema tayari watu wanne waliokuwa katika mtandao
huo wa ujambazi wamefikishwa mahakamani kwa mashitaka ya unyang'anyi na
mauaji.
Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni pamoja na Kyoma Manguh, Marwa Mwita , Yohana Mgosi na Chacha
Bugichere ambapo kesi zao zitatajwa Februari 19 mwaka huu.
Jana mamia ya wananchi wilayani Tarime walifurika kuona mwili wa
Kichune maarufu Kenonke ambaye amekuwa tishio kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Polisi imetangaza zawadi ya Sh milioni moja kwa
atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamata silaha za moto katika wilaya za Tarime na Rorya.
No comments:
Post a Comment