Wamiliki wa Kampuni za Kusambaza Mbegu za Pamba na Dawa za kuua wadudu Kanda ya Ziwa, wamekamatwa na polisi ndani ya mkutano wa kawaida wa wadau wa bodi ya pamba, uliofanyika jana katika ukumbi wa halmashauri wilayani hapa mkoani Geita kwa tuhuma za kuhujumu zao hilo.
Hatua hiyo imekuja kutokana na agizo la Mwenyekiti
wa Bodi ya Pamba ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Saidi Magalula kwa kile
alichodai wamiliki hao wamekiuka agizo la Serikali walilokubaliana
kuwakopesha wakulima dawa za kuua wadudu, jambo lililomlazimu kuita
polisi na kuwakamata wakati mkutano huo ukiendelea.
“Msitufanye sisi wajinga, tumekaa vikao vingi hapa
tukakubaliana kwamba mkawakopeshe wakulima dawa na mbegu, badala yake
mkakataa na kuanza kuwauzia, DC naomba umwite OCD wakatoe maelezo
polisi,” alisema Magalula.
Wamiliki hao waliingia mkataba na Serikali Octoba
mwaka jana kwa makubaliano na Bodi ya Pamba kwamba iwakopeshe wamiliki
hao mbegu na dawa na kisha kampuni hizo zikatoe mikopo kwa wakulima kwa
lengo la kuinua uzalishaji wa zao hilo lakini badala yake kampuni hizo
zilikopeshwa mbegu na bodi lakini wao wakaenda kuwauzia wakulima.
“Sisi tuliwakopesha dawa na mbegu na tukakubaliana
mtaenda kuwakopesha wakulima, lakini nyie mkafanya biashara na pesa
mkaweka mifukoni, huo ni wizi wa mchana kweupe na sisi hatutawanyamazia,
naomba mkatoe maelezo polisi, OCD kamata hao peleka polisi,” alisema
Magalula.
Aidha wakizungumza kwa nyakati tofauti kabla
hawajakamatwa wakati wakihojiwa na viongozi wa bodi kama wanataka ama
hawataki kuwakopesha wakulima, walikana kuwa wao hawajakataa kuwakopesha
wakulima isipokuwa wakulima ndiyo walikataa kukopa .
“Sisi hatujakataa kuwakopesha wakulima wenyewe
ndiyo hawakuwa tayari kukopa,” alisema Wiliam Matonange Meneja wa
Kampuni ya Kahama Oil Mills Limited .
Aidha Magalula alisema, wakulima hawajakataa
kukopeshwa na taarifa zote wanazo kwamba kampuni hizo ndizo zilikataa
kuwakopesha licha ya kuwa wao walikopeshwa na bodi.
“Msitupotezee muda kama hamtaki mseme hatutaki,
nyie kama watu wazima mmeniudhi sana, hivyo sitaki maelezo mkatoe
polisi,” alisema Magalula.
Baadhi ya kampuni zinazodaiwa kushindwa kukopesha
wakulima hao ni pamoja na Kahama Cooperative Union (KAW) LTD, Kahama Oil
Mills Ltd na Fresho Inuco Ltd.
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment