Baada
ya baadi ya viongozi kuanza kutangaza nia ya kugombea urais mwaka 2015
sasa serikali imetoa onyo na pia imeanza kuwabana wafanyakazi ili
wasikiuke maadili ya kazi.
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome Kaganda wa kwanza (kulia) Picha na Maktaba
Suala
la baadhi ya viongozi nchini kuanza kampeni za kuwania urais mwaka 2015
kwa kumwaga fedha ili kujijengea mazingira ya ushindi, limechukua sura
mpya baada ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuanza
kuwabana.
Habari
zilizolifikia gazeti hili na baadaye kuthibitishwa na Kamishna wa
Sekretarieti hiyo, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, zinaeleza kuwa chombo
hicho cha Serikali tayari kimewaita watu hao na kuwapa onyo baadhi yao
wakiwamo mawaziri na wabunge walioanza kufanya kampeni.
Jaji
Kaganda alisema kuwa waliwaita baadhi ya wanasiasa hao ambao wengi wana
hadhi ya ubunge na kuwaonya kutokana na kubainika kwamba wanakiuka
kanuni za maadili.
“Kwa
upande wetu tumeshawaita baadhi, tulizungumza nao na kuwaonya kuhusu
nyendo zao. Wapo waliotuelewa, naona wamekuwa kimya wakiendelea na
shughuli zao nyingine za ujenzi wa taifa kwa nyadhifa walizonazo, ingawa
pia wapo wengine tunasikia wanaendelea,” alisema Jaji Kaganda.
Tayari
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepanga kuwachukulia hatua baadhi ya
makada wake wanaodaiwa kuanza kufanya kampeni kabla ya wakati.
Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula wiki hii alikaririwa akiwa mjini
Morogoro akisema kwamba tayari wamefungua mafaili ya watu wenye mitandao
ya kampeni akisema wanaitambua mitandao hiyo hadi ngazi za mikoa na
wataishughulikia.
Alisema kuwa muda wa kampeni za urais, udiwani, ubunge haujafika, hivyo wanaofanya kampeni sasa wanakiuka Katiba na Kanuni.
Kwa
upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,
alipoulizwa kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaodaiwa kujipitisha
kabla ya muda wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, alisema ofisi yake ipo
tayari kuwashughulikia kwa mujibu wa utaratibu, ikiwamo kuwashtaki
kwenye Sekretarieti ya Maadili, iwapo barua za malalamiko zitafikishwa
kwake.
“Kwa
jambo hili hatuwezi kuchukua hatua yoyote kama hakuna barua ya
malalamiko iliyoletwa kwetu, hasa na vyama husika. Hivi sasa na sisi
tumebaki tunaona na kusikia tu kwenye vyombo vya habari,” alisema Jaji
Mutungi.
Wiki
iliyopita wabunge wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria walipokuwa
kwenye ziara kwenye Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili, walihoji jinsi
chombo hicho cha umma kilivyojipanga kuwashughulikia viongozi wanaodaiwa
kumwaga fedha wakiwa katika maandalizi ya kugombea urais na ubunge.
Wabunge
Mjumbe
wa Kamati hiyo, Nyambari Nyangwine ambaye pia ni Mbunge wa Tarime,
alitaka kujua jinsi Sekretarieti hiyo, inavyoweza kuwashughulikia
viongozi hao kwa kuwa vitendo hivyo vinakiuka maadili ya uongozi.
“Sekretarieti
itawashughulikia vipi watu hawa ambao katika kuelekea Uchaguzi Mkuu,
wameanza kampeni, wanamwaga fedha ili wapate uongozi?” Alihoji mbunge
huyo.
Akijibu
swali hilo, Katibu wa Utumishi wa Sekretarieti hiyo, Tixon Nzunda,
alisema jukumu lao ni kushughulikia watu ambao tayari wana hadhi ya
uongozi na kwamba zipo pia taasisi nyingine za Serikali zinazoweza
kulifanyia kazi suala hilo.
“Ila
pia kuna taasisi ambazo zinapaswa kuchukua hatua dhidi ya jambo hilo,
kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema.
Aliongeza:
“Sisi kwa upande wetu tumekuwa tukishirikiana na vyama hivyo, kwa
kuwasisitizia viongozi wao kuhakikisha wanateua wagombea walio na sifa
za maadili ili kulinda heshima na maana ya uongozi.”
Kuhusu
Sheria ya Kutenganisha Uongozi na Biashara, ambayo baadhi ya wajumbe wa
kamati hiyo waliomba itazamwe upya, alisema mtu anayetaka kuwa
kiongozi, anatakiwa kuepuka mambo yanayoweza kusababisha mgongano wa
kimasilahi.
“Unapokuwa
kiongozi lazima uyatambue mazingira yanayoweza kukusababishia mgongano
wa kimasilahi, hivyo hatua hiyo ya kuzuia viongozi kuwa wafanyabiashara,
siyo kwa sababu ya Azimio la Arusha, bali inalinda pia maadili ya
kiongozi,” alisema Nzunda na kuongeza;
“Hata
hivyo, kuna mambo ambayo kiongozi mfanyabishara anatakiwa kuchagua moja
kati ya matatu ambayo ni kuuza hisa zake katika kipindi cha siku 90
tangu kuchaguliwa, au aipeleke kwenye taasisi atakayoiamini na ajiondoe
kusimamia au asikubali kuwa kiongozi.”
Akitoa
ufafanuzi juu ya hilo, Jaji Kaganda alisema, viongozi hawakatazwi kuwa
matajiri, isipokuwa wanapaswa kujipatia mali kwa njia halali, kwa kuwa
wakiwa na uwezo wa kipato, pia husaidia kutatua matatizo madogo ya watu
wanaowaongoza.
“Naomba
muelewe vyema, haikatazwi kiongozi kuwa tajiri, kwa sababu napo
kiongozi akiwa maskini hataweza kuwasaidia wananchi kutatua matatizo
yanayogharimu, hata kwa Sh10,000,” alisema.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment