WAZIRI mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema mahali popote penye uchumi dhaifu hata utawala bora hauwezi kupatikana mahali hapo.
Akizungumza na jumuiya ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu jijini Mwanza, katika kongamano lililoandaliwa na serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Biashara (COBESO) Mwanza jana katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Chama cha Ushirika Nyanza, Sumaye alisema uchumi dhaifu huweza hata kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuwa ni rahisi sana kusababisha mifarakano ndani ya jamii, kwa sababu jinsi watu wanavyokuwa na maisha magumu, ndivyo wanavyokuwa hawaridhiki.
Kwa mujibu wa Sumaye, uchumi dhaifu huweza kusababisha hasira za muda wote za wananchi dhidi ya serikali yao au hata baina yao wenyewe kwa wenyewe, na hasa panapokuwa na tofauti kubwa ya hali za maisha.
“Upungufu wa huduma inayosababishwa na uchumi duni, hufanya huduma chache zilizopo kupatikana kwa njia za rushwa na upendeleo, na kwa hiyo penye uchumi dhaifu hata utawala bora ni nadra sana kuwepo,” anasema Sumaye.
TUNAOMBA BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI MOTOMOTO(USIPITWEEEE)
Sumaye, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo wa COBESO, aliyasema hayo katika mada yake aliyoitoa kwa wanafunzi hao na jumuiya nzima ya chuo hicho katika mada yake aliyoipa jina la Ujenzi na Ukuaji wa Uchumi Imara.
Awali, wanafunzi hao wa CBE Mwanza, walikuwa wamemtaka Sumaye, kuzungumzia mada juu ya Maendeleo ya Vijana na Tatizo la Ajira. Hata hivyo, waziri mkuu huyo mstaafu aliamua kugeuza kidogo mada hiyo kwa kuipa uzito zaidi, na kuifanya iwe Ujenzi na Ukuzaji wa Uchumi Imara kutokana na sababu kadhaa.
Alisema pamoja na kwamba tatizo la ajira, na hasa ajira kwa vijana ni agenda kubwa katika nchi nyingi duniani, Tanzania ikiwemo, lakini tatizo hilo ni matokeo (symptom) tu ya tatizo kubwa na la msingi la uchumi usiokidhi haja.
“Ni vizuri kuzungumzia ugonjwa wa malaria na matibabu yake badala ya kutibu joto la homa linalotokana na ugonjwa wa malaria,” alisema Sumaye na kuongeza: “Kwa sababu chuo hiki ni cha biashara, hivyo malengo yake mapana yanafanana zaidi na ukuzaji wa uchumi kuliko ajira tu.”
Akizungumzia uchumi imara, Sumaye alisema uchumi ni kielelezo muhimu sana kinachotoa taswira halisi ya nchi husika na kwamba nchi zenye uchumi imara, huwa na maendeleo mazuri ya watu wao na watu huwa na maisha mazuri na kufanya shughuli zao katika hali ya kujiamini.
“Katika nchi zenye uchumi imara, serikali huwa na uwezo mzuri wa kutoa huduma nzuri kwa jamii kwa viwango vizuri, na kwa sababu hiyo matatizo kama ya rushwa, huwa madogo sana kama yapo. Nchi zenye uchumi dhaifu mara nyingi ni masikini, ambapo watu wao huishi katika mazingira magumu na serikali husika haiwezi kuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu kwa watu wake kwa viwango vinavyotakikana,” anasema Sumaye.
Kwa mujibu wa Sumaye, ili taifa lolote liweze kuwa na uchumi imara, lazima nguzo kuu za uchumi mkuu nazo ziwe imara pia. Alivitaja viashiria vya nguzo kuu hizo za kiuchumi kuwa ni pamoja na mfumko wa bei ambao lazima uwe chini kadri inavyowezekana ili biashara ya nje ikue, unafuu wa gharama za maisha, ukuaji wa uchumi wa taifa ulioendelevu, uwiano mzuri wa biashara kati ya bidhaa zinazonunuliwa nje na zinazouzwa nje, thamani ya fedha ikilinganishwa na sarafu kuu ulimwenguni na kadhalika.
“Vigezo na viashara hivi ni vitu muhimu sana kwa uchumi ulio imara na unaokua, vinginevyo uchumi wa nchi utayumba na hautaaminika ili watu wa nje na ndani waweze kuwekeza bila wasiwasi,” alisisitiza Sumaye.
Kutokana na hali hiyo, Sumaye alisema ili kuwe na uchumi imara katika taifa lolote, lazima uchumi huo uanzie kwenye nguzo kuu za uchumi wa ndani zilizo imara, ambazo zinamwezesha mtu mmoja mmoja au ngazi ya familia katika nchi kumudu naisha yake na kupata huduma muhimu na bora karibu yake.
“Muhimu hapa ni kuona kuwa matunda ya uchumi imara yanamfikia kila mmoja anayefanya kazi kwa bidii. Sehemu hii ya uchumi isiposimamiwa vizuri, unaweza ukapata hali ambapo kitakwimu uchumi unakua, lakini sehemu kubwa ya wananchi ni masikini sana, na utajiri unaoonekana kwenye takwimu hizo uko mikononi mwa wachache tu…ni lazima uchumi wa ndani umnufaishe kila mtu na wananchi wapate huduma wanazostahili bila vikwazo.” Alisema.Chanzo Gazeti la Raia Mwema
No comments:
Post a Comment