Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, February 21, 2014

TAARIFA ZA KIMICHEZO KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

tff_LOGO1

TWIGA STARS, ZAMBIA SASA KUCHEZA FEB 28
Mechi ya pili ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Zambia (Shepolopolo) sasa itachezwa Februari 28 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Twiga Stars tayari ipo kambini kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex.
Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe. Zimbabwe ilishinda mechi ya kwanza ugenini
Wachezaji wa Twiga Stars waliopo kambini ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya, Fatuma Mustafa, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Flora Kayanda, Happiness Mwaipaja, Maimuna Mkane, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Pulkeria Charaji, Sherida Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.
MECHI TANO VPL KUCHEZWA JUMAMOSI
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 19 kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Bukoba, Morogoro, Tanga na Arusha.
Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting ya mkoani Pwani katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Nayo Kagera Sugar inaikaribisha Rhino Rangers ya Tabora katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Uwanja wa Manungu uliopo Turiani mkoani Morogoro ndiyo utakaotumika kwa mechi kati ya Mtibwa Sugar na Ashanti United, wakati Coastal Union itaumana na Mbeya City katika mechi itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kutoka Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Maafande wa Oljoro JKT watakuwa nyumbani kupambana na Mgambo Shooting katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
Jumapili (Februari 23 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa ni Simba dhidi ya JKT Ruvu, mechi ambayo pia itaoneshwa moja kwa moja na Azam Tv. Mechi kati ya Azam na Tanzania Prisons iliyokuwa ichezwe kesho (Februari 22 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi sasa itachezwa Jumapili (Februari 23 mwaka huu) ambapo na itakuwa ‘live’.
Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Februari 26 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ashanti United na Azam itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex (Chamazi).

MICHUANO YA MIKOA KUSAKA VIPAJI YATIMUA VUMBI
Michuano ya mikoa katika mpango maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuboresha Taifa Stars inaanza kutimua vumbi kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi nne.
Mechi rasmi ya ufunguzi wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kati ya Ilala na Temeke. Mechi hiyo ya kundi G itachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia saa 9.30 alasiri.
Kundi A kutakuwa na mechi kati ya Pwani na Morogoro kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Kusini Unguja na Kaskazini Unguja zitacheza kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung mjini Unguja katika kundi F
Kusini Pemba na Kaskazini Pemba zitacheza mechi ya Kundi I katika Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.
Mechi za keshokutwa (Februari 23 mwaka huu) ni Simiyu itacheza na Shinyanga mjini Bariadi katika kundi E. Nayo Ruvuma itacheza na Njombe kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea katika kundi D.
Kundi C ni Tanga na Kilimanjaro kwenye Uwanja wa Mkwakwani wakati Kagera itacheza na Geita kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba katika kundi B. Mtwara itacheza na Lindi kwenye Uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara katika kundi F.
Wang’amuzi 40 wa vipaji tayari wamesharipoti kwenye vituo vya mechi hizo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika Jumatatu (Februari 24 mwaka huu).
Mkutano huo utafanyika saa 6 kamili mchana kwenye ofisi mpya za TFF zilizopo ghorafa ya tatu katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Garden na Ohio jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment