Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Jamali Malinzi, (kushoto) akimkabidhi Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Msanifu Kondo (kulia) jezi kwa ajili ya Ligi ya Taifa inayotarajiwa kuanza Februari 22, mwaka huu katika kanda tisa |
MASHINDANO
maalumu ya mikoa ya kuunda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa
Stars’ yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Februari 22 hadi Machi 5 mwaka
huu, huku ikiigharimu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) takribani Sh.
Milioni 360.
Michuano
hiyo maalumu itashirikisha mikoa wanachama ya TFF na itakuwa ikichezwa
kwa mfumo wa nyumbani na ugenini kwa timu mbili za kanda moja kuchuana
na inatarajiwa kutoa wachezaji bora 60 wataoweka kambi ya siku 30
Tukuyu, Rungwe mkoani Mbeya
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF Jamal
Malinzi amesema michuano hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuuunda upya
kikosi bora cha Stars, ili kiweze kufuzu kwa fainali za Mataifa ya
Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwakani nchini Morocco.
Malinzi
alisema jumla ya timu 32 za Tanzania nzima zitashiriki michuano hiyo,
kila mechi moja watakuwepo wasaka vipaji watano ‘Scouts’ kwa ajili ya
kumulika wachezaji bora, pia mechi zote zitakuwa zikirekodiwa.
Baada
ya zoezi la kuibua vipaji kwenye michuano hiyo, wasaka vipaji wote
watajifungia (retreat) kwa muda wiki moja mjini Lushoto, Tanga kupitia
rekodi zote za mechi na kuchagua wachezaji 60 bora, ambao watapelekwa
Tukuyu, Mbeya kwa ajili ya mazoezi makali na wataalamu mbalimbali.
Wachezaji
hao 60 watachujwa baada ya mwezi mmoja na kubaki 30, ambao
watachanganywa na wachezaji wa sasa wa Taifa Stars na baadaye kupatikana
kikosi bora kwa ajili ya mapambano ya kuwania kufuzu kwa AFCON.
Malinzi
alisema wachezaji wa sasa wa Stars nao watakwenda kwenye kambi hiyo
mkoani Mbeya mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
mwezi Aprili.
“Tunaamini
mfumo huo utasaidia kupata vijana wapya wa kuboresha kikosi cha Stars,
hatutachagua majina wala kuangalia umri kwa kuwa hiki ni kipindi cha
mpito na ni muda mchache umebakia kuelekea kwenye michuano hiyo,”
alisema Malinzi.
Machi
5 mwaka huu Stars itashuka dimbani kuumana na Namibia katika mechi ya
kirafiki inayotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
No comments:
Post a Comment