Vigogo
sita ambao wanatajwa kuwa wanajiwinda kwa ajili ya kuwania urais kupitia
CCM katika uchaguzi mkuu ujao, wameitwa mbele ya Kamati ya Ndogo ya
Maadili ya chama hicho, kwa ajili ya kuhojiwa kwa tuhuma za kukiuka
maadili.
Habari
ambazo zililifikia gazeti hili jana zinawataja vigogo hao kuwa ni Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano
na Uratibu), Steven Wassira na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine
ni Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
“Wote
wamepelekewa barua za wito wa kufika mbele ya Kamati ya Maadili
inayoongozwa na Mzee Mangula (Philip, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara),
ambayo itakutana mjini Dodoma, Februari 14 (kesho kutwa) ,” kilisema
chanzo chetu cha habari kutoka Ofisi Ndogo ya CCM, Lumumba, Dar es
Salaam na kuongeza:
“Barua
hizo zimesainiwa na Mzee Kinana (Abdulrahman, Katibu Mkuu wa CCM)
mwenyewe na tayari zimeanza kusambazwa leo (jana) mchana.”
Kamati
hiyo ndogo ya maadili, inaundwa na Mangula, Kinana, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Shamsi
Vuai Nahodha, Dk Maua Daftari na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye jana alithibitisha kuwapo kwa
Kikao cha Kamati ya Maadili Februari 14 pamoja na kuitwa kwa baadhi ya
wanachama kwa ajili ya kuhojiwa.
Haa
hivyo, hakuwa tayari kutaja majina yao wala idadi ya walioitwa... “Wewe
fahamu tu kwamba kikao hicho kitafanyika tarehe hiyo uliyoitaja, lakini
masuala ya majina na idadi ya walioitwa yatajulikana kwenye kikao, mimi
sina kwa sasa,” alisema Nnauye.
Katika
siku za karibuni kumekuwa na vita ya maneno baina ya makada wa chama
hicho, wakituhumiana kutangaza mapema kugombea urais kabla ya ruhusa
rasmi ya chama.
Kauli za walioitwa
Jana, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya walioitwa na wengi wao walisema hawakuwa wamepokea barua za wito huo.
Sumaye kwa upande wake alisema: “Kwa sasa niko Mwanza na sijapata barua yoyote ya kuitwa katika kikao chochote cha chama.”
Lowassa
alipigiwa simu mara kadhaa na kusema kuwa yuko kwenye kikao apigiwe
baadaye. Alipigiwa mara sita na kusema alikuwa bado kwenye kikao.
Membe kwa
upande wake alisema: “Kwangu si mara ya kwanza kuitwa Kamati ya
Maadili, ifahamike kwamba unaweza kuitwa kutoa ushahid, maelezo au
ufafanuzi wa jambo lolote unalokuwa umeitiwa.”
Wassira
pia alisema hakuwa amepata barua hiyo ya wito... “Mimi ndiyo nimeshuka
kutoka Bunda, sina hiyo barua ya kuitwa kwenye Kamati ya Maadili.
Mwaliko nilionao ni wa kikao cha Kamati Kuu kesho (leo) ambao mimi ni
mjumbe,” alisema Wassira.
Kwa
upande wake, Makamba naye alisema alikuwa hajapata wito huo, wakati
Ngeleja hakukanusha au kuthibitisha kupokea barua hiyo kwa maelezo
kwamba yeye siyo msemaji wa CCM, hivyo asingeweza kuzungumzia suala la
kuitwa kwake.
“Kwa
kweli wewe fahamu tu kwamba mimi siyo msemaji wa chama. Chama chetu kina
utaratibu wa wasemaji wake, waulize hao maana watakuwa na taarifa
sahihi,” alisema Ngeleja.
Katika
hatua nyingine, Nnauye alisema Kamati Kuu (CC) ya CCM, inakutana Dar es
Salaam leo, huku Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ikitarajiwa
kukutana Jumamosi na Jumapili wiki hii mjini Dodoma.
Vikao
hivyo pamoja na mambo mengine vinatarajiwa kujadili ushiriki wa wajumbe
wake katika Bunge Maalumu la Katiba ambalo limepangwa kuanza Februari
18, mwaka huu mjini Dodoma.NA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment